WAKATI Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka, ametoa siku 30 za kuvunjwa kwa jengo la ghorofa 17 lililoko
mtaa wa Indila Ghandi, Dar es Salaam, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu, Aggrey Mwanri, amezuia kuvunjwa kwa jengo hilo hadi uchunguzi
utakapokamilika.
Kauli hizo za kupishana zilibainika bungeni jana wakati Naibu Waziri
Mwanry alipojibu swali la nyongeza la mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia
(NCCR-Mageuzi).
Katika swali lake, Mbatia alitaka kujua kuhusiana na jengo pacha
lililoko mtaa wa Indila Ghandi ambalo wakati wowote linaweza kuleta
maafa kutokana na kupaswa kujengwa ghorofa tisa, lakini limejengwa
ghorofa 17.
Pia Mbatia aliitaka serikali kutoa kauli ya kuamuru kubomolewa kwa jengo hilo mara moja.
Akiendelea kujibu swali hilo, Mwanri alisema hawezi kutolea jibu la
moja kwa moja kuhusu suala hilo, ila wanalifuatilia jengo hilo ili
waweze kubaini ukweli na endapo wataridhika watatoa kauli, jibu ambalo
liliungwa mkono na Spika, Anna Makinda, ambaye alisema kama angetoa
kauli ya kuamuru kuvunjwa kwa jengo hilo wangemshangaa.
Katika swali la msingi, mbunge wa Magomeni, Muhamad Amour Chombo
(CCM), alitaka kujua serikali ilivyojiandaa katika miundombinu ya
majisafi na majitaka, umeme na barabara za mitaa husika, ili kukidhi
mahitaji ya lazima kwa wakazi wa mitaa hiyo.
Akijibu swali hilo, Mwanri alikiri kuwepo na ongezeko kubwa la ujenzi
wa nyumba za ghorofa katika jiji la Dar es Salaam unaotokana na ukiukaji
wa shughuli za kiuchumi na kijamii.
“Ongezeko hili limeleta changamoto za miundombinu ya majisafi na
salama kutokidhi mahitaji, uzalishaji mkubwa wa taka ngumu na majitaka,
uzalishaji na usambazaji mdogo wa umeme usiokidhi, mahitaji, pamoja na
mtandao mkubwa wa barabara ambazo hazijajengwa kwa kiwango cha lami,”
alisema Mwanri.
Alisema ili kukabiliana na changamoto za miundombinu duni isiyoendana
na ongezeko la watu na makazi, serikali imeanza kutekeleza mipango
mbalimbali ikiwemo ya uboreshaji wa miundombinu kupitia mradi wa Dar es
Salaam ‘Metropolitan Development Projrect’ (DMDP) kwa mkopo wa dola
milioni 75 za Marekani kutoka Benki ya Dunia.
Alisema mradi mwingine ni wa mabasi yaendayo kasi Dar es Salaam (Dar
es Salaam Rapid Transit) unaojengwa kwa dola milioni 281.22 ambazo ni
mkopo wa Benki ya Dunia, mchango wa serikali kuu na sekta binfsi.
No comments:
Post a Comment