TISHIO la ugaidi linaloikabili Tanzania limechukua sura mpya
baada ya vyombo vya ulinzi kwa kushirikiana na maofisa usalama
kulazimika kukesha wakifanya doria mjini hapa kuhakikisha ibada ya
kusimikwa kwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana (KKKT), Dk. Jacob
Chimeledya inafanyika salama.
Ulinzi huo uliendelea kutwa nzima jana kuzunguka Kanisa Kuu la
Anglikana mjini hapa na maeneo jirani wakati wote wa ibada hiyo
iliyohudhuriwa na Askofu Mkuu wa Cantebury nchini Uingereza, Justin
Welby huku Rais Jakaya Kikwete akiwa mgeni rasmi.
Tangu juzi usiku maofisa wa polisi waliovalia sare na kiraia pamoja na
wale wa usalama walikuwa wakizunguka katika mitaa mbalimbali ya mjini,
kuzunguka kanisa kuu hilo huku baadhi yao wakiwa na silaha za moto na
mbwa.
Wakati wote ibada ikiendelea jana, barabara ya kutoka soko kuu la
Majengo kupitia hospitali ya rufaa ya mkoa ilikuwa imefungwa huku ile ya
kutoka Hoteli ya Dodoma hadi Nyerere ikiwa imefurika askari
waliosheheni silaha.
Tofauti na ibada nyingine za siku zote, jana waumini waliohudhuria
walilazimika kupekuliwa kwa umakini zaidi na maofisa usalama na kwa
waumini waliokuwa na pochi na mikoba walitakiwa kufungua na kuonesha
vitu vilivyomo licha ya kupitishwa katika mashine maalumu.
Tahadhari kwa vitisho hivyo vya kigaidi imenza kuchukuliwa kwa umakini
zaidi na vyombo vya dola baada ya matukio ya mashambulizi ya kigaidi
yaliyotokea Zanzibar kwa viongozi wa dini kushambuliwa na lile la hivi
karibuni la kulipuliwa kwa Kanisa Katoliki Parokia ya Olasiti jijini
Arusha.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nalo limechukua tahadhari kwa
kuwazuia wabunge kuegesha magari yao nje ya uzio wa Bunge na badala
yake wawe wanayaegesha ndani au mkabala na jengo ng’ambo ya barabara ya
Dodoma-Dar.
Akizungumzia vitendo hivyo vya ugaidi muda mfupi baada ya kusimikwa,
Askofu Dk. Chimeledya alisema kuwa bado tatizo hilo linaonekana kuchukua
nafasi kubwa, jambo ambalo linatishia amani ya Watanzania.
“Vitendo vya ugaidi vinaonekana kushamiri nchini na kulichafua taifa
letu, na serikali lazima ioneshe juhudi za makusudi kuhakikisha watu
ambao wanahusika na vitendo hivyo wanachukuliwa hatua.
“Hali hii ni mbaya na kwa siku za karibuni yametokea matukio mabaya
sana kwa viongozi wa makanisa. Hii inasikitisha na inatia aibu kwa taifa
letu ambalo limezoea amani, upendo na mshikamano,” alisema.
Alisema serikali inatakiwa kutambua kuwa hali ya kisiasa kwa sasa ni
mbaya katika nchi pamoja na dunia kwa ujumla na watu wanaonekana kukata
tamaa ya kuendelea kutawaliwa kutokana na kusongwa na umasikini ambao
unaonekana kuwatesa.
Askofu Dk. Chimeledya alisema inasikitisha kuona kuwa nchi ina
rasilimali nyingi lakini bado hazitumiwi na wazawa na badala yake kuna
watu wachache kutoka mataifa mengine wanaokuja na kuzichukua kwa
kujitajirisha huku wananchi wanaendelea kuwa masikini.
“Lazima serikali ichukue hatua kuhakikisha inakomesha mara moja
vitendo vya baadhi ya watu wa kutoka nje kujichukulia rasilimali huku
Watanzania wakiwa masikini,” alisema.
Akizungumzia malengo ya kanisa hilo, Dk. Chimeledya alisema
limejipanga kujenga vyuo vikuu katika mikoa ya Kigoma na Mtwara pamoja
na benki ambayo itakuwa na manufaa kwa Watanzania wote.
Askofu Mkuu wa Cantebury, Welby, alisema serikali inatakiwa kufanya
kazi kwa ushirikiano mkubwa na viongozi wa dini badala ya kuwagawa.
“Serikali ina kila sababu ya kuhakikisha inafanya kazi za kimaendeleo
kwa ushirikiano mkubwa na viongozi wa dini. Ikumbukwe viongozi wa dini
wana mchango mkubwa wa kimaendeleo kwa sekta zote kielimu, kiafya pamoja
na kihuchumi,” alisema.
JK aonya
Rais Kikwete akizungumza katika ibada hiyo, alisema kuwa serikali
itahakikisha inawasaka wote ambao walijihusisha na vitendo vya uvunjifu
wa amani kwa kuhusika na ugaidi.
Alisema pamoja na kujitokeza kwa vitendo vya kihuni ambavyo vinafanywa
na baadhi ya watu wachache kwa lengo la kutowesha amani, lakini
serikali kwa kutumia vyombo vya ulinzi na usalama watahakikisha
wanawasaka.
“Ni aibu kuona serikali ambayo waasisi wake walijenga misingi ya
upendo, umoja na mshikamano lakini kutokana na watu kuwa na matakwa yao
binafsi wanatumiwa ama wanajisikia kuvunja hali ya utulivu.
“Nataka kusema kuwa vitendo hivi vya kigaidi vinachochewa na kikundi
cha watu wachache ambao kimsingi wao wanajua yakitokea machafuko kamwe
hawawezi kukaa hapa nchini, watakimbilia nje,” alisema Kikwete.
Alitolea mfano wa wananchi wanaotoka mikoa inayopakana na mataifa
jirani akisema kuwa vurugu zikitokea wao watakimbilia huko wakati wale
wasio na uwezo huo wakitaabika.
“Wapo watu ambao yakitokea machafuko hapa nchini wao hawaoni tatizo,
mfano James Mbatia yeye atakimbilia Kenya, Profesa Anna Tibaijuka yeye
atakimbilia Uganda. Lakini wale ambao hawana pa kukimbilia mnafikiria
watakimbilia wapi?” alihoji.
Aidha alizitaka dini zote kuhakikisha zinaiombea serikali na wale wote
ambao wana roho ya uharibifu kuacha tabia hiyo na badala yake watunze
amani iliyopo.
Pia alizigeukia dini alizodai zinaonekana kuwa na viashiria vya uchochezi na kusema kuwa dini hizo ni sawa na mashetani.
Rais Kikwete alisema kuwa anatambua mchango wa makanisa katika kuwasaidia Watanzania kihuchumi, kiafya na kielimu.
No comments:
Post a Comment