Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu Mkuu (Ofisi ya Waziri Mkuu), Peniel Lyimo
Serikali imesema hali ya lishe nchini hairidhishi na
kwamba asilimia 42 ya watoto walio na umri chini ya miaka mitano
wamedumaa, asilimia 16 wana uzito pungufu wakati asilimia tano
wamekonda.
Aidha, asilimia 11 ya wanawake walio katika umri wa kuzaa yaani miaka 15 hadi 49 wamekonda wakati asilimia 58 ya wajawazito wana upungufu wa damu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Peniel Lyimo, alisema hali hiyo inapunguza kasi ya Taifa ya maendeleo.
Alisema tatizo la utapiamlo linaendelea kuongezeka na linaathiri zaidi wakazi wa vijijini na kwamba linachangia kuwepo magonjwa yasiyoambukiza kama ya moyo, kisukari na saratani.
Lyimo ambaye pia ni Katibu Mkuu (Ofisi ya Waziri Mkuu), alisema tatizo la lishe linaanza tangu mtoto anapokuwa tumboni hadi siku 1,000 za mwanzo baada ya kuzaliwa na kwamba utapiamlo unaathiri ukuaji wa mtoto kiakili na kimwili; madhara ambayo hayawezi kurekebishwa.Hata hivyo, alisema serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwamo kuanzisha madawati ya lishe kwenye Halmashauri zote nchini na mkakati wa sasa wa kuongeza virutubishi kwenye unga na mafuta ya kula.
Alisema Rais Kikwete atazindua kampeni hiyo ya kitaifa Mei 16 mwaka huu, katika viwanja vya Mnazi Mmoja baada ya kufanya ziara kwenye viwanda vinavyozalisha mafuta na unga Mei 15.
Wakati huo huo, Mshauri wa Rais wa Masula ya Lishe, Dk. Wilibrod Lorri, alitaja mikoa inayoongoza kwa utapiamlo kuwa ni Kagera, Mbeya, Kigoma, Iringa, Arusha, Lindi, Shinyanga, Tanga, Morogoro, Manyara, Mtwara, Rukwa, Ruvuma na Dodoma.
Mingine ni Singida, Mwanza, Pwani, Tabora, Pwani, Mara, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba.
No comments:
Post a Comment