Idadi ya watuhumiwa wa tukio la kulipua bomu katika
Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, mkoani Arusha
Jumapili iliyopita, imeongezeka kutoka tisa hadi 12.
Sasa wafikia 12, jalada lapelekwa kwa DPP
IGP Mwema atangaza bingo ya Sh. milioni 50
IGP Mwema atangaza bingo ya Sh. milioni 50
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas.
Watuhumiwa hao wametajwa na Jeshi la Polisi kuwa ni Victor Ambrose Kalisti (20) na Joseph Yusuph Lomayani (18), ambao wote ni waendesha bodaboda wakazi wa Kwa Mrombo, mkoani Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, aliwataja watuhumiwa wengine wanaoshikiliwa kuwa ni George Batholomeo Silayo (23), ambaye ni mfanyabishara na mkazi wa Olasiti; Mohamed Sulemani Said (38) mkazi wa Ilala, mkoani Dar es Salaam, ambaye polisi imemtaja kuwa ni mwenyeji wa watuhumiwa raia wa Uarabuni na kwamba ndiye aliyewafuata kwa gari binafsi uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam na kuwachukua hadi Arusha katika hoteli moja iliyoko karibu na kituo kikuu cha mabasi yaendayo mkoani humo na nje ya mkoa.
Wengine wanaoshikiliwa ni Said Abdallah Said (28), ambaye ni raia wa Falme za Kiarabu, katika mji wa Abudhabi; Abdulaziz Mubarak (30), ambaye ni mkazi wa Saudi Arabia; Jassini Mbarak (29), ambaye ni mkazi wa Bondeni Arusha; Foud Saleem Ahmed (28), ambaye ni raia wa Falme za Kiarabu na Said Mohsen, ambaye ni mkazi wa Najran Falme za Kiarabu.
IGP ATOA BINGO YA SH. MILIONI 50
Aidha, Jeshi la Polisi nchini kupitia Mkuu wake, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, limetangaza donge nono la Sh. milioni 50
kwa mtu yeyote atakayefanikisha kufichua mtandao wa kigaidi nchini.
Kamanda Sabasi alisema hayo alipokuwa akitoa taarifa kuhusu hatua zilizochukuliwa tangu kutokea kwa mlipuko wa bomu hilo Jumapili saa 4.30 asubuhi kwenye kanisa hilo.
Kamanda huyo ambaye jana alizungumzia tukio hilo kwa mara ya kwanza, alisema siku ya tukio kulikuwa na uzinduzi wa kanisa hilo na mgeni rasmi alikuwa Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Francisco Padilla, na alipokuwa akijiandaa kukata utepe kama ishara ya uzinduzi, ghafla mtu mmoja aliyejificha kwenye choo cha jirani, upande wa Kaskazini, alirusha kitu kizito.
Kamanda Sabas alisema kitu hicho kilirushwa umbali wa mita 20 na kilikuwa na ukubwa wa ngumi ya mtu mzima, kuelekea kwenye mkusanyiko wa waumini na kilipotua chini ulitokea mlipuko mithili ya bomu na kusababisha watu 66 kujeruhiwa, ambao kati yao watatu walipoteza maisha.
Alisema watuhumiwa hao bado wanaendelea kuhojiwa na tayari jalada la mashtaka dhidi yao limepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kwa ajili ya maamuzi ya kisheria.
Kamanda Sabas alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa bomu hilo siyo la kienyeji na pia wageni hao walikuwa na VISA halali ya kukaa nchini, kwa madai kuwa walikuja harusini.
“Watuhumiwa hawa wa Falme za Kiarabu tulipowahoji, walidai wamekuja harusini, lakini tunaendelea nao,” alisema.
Alisema watuhumiwa watatu wanaendelea kuhojiwa na kwamba kutokana na hali hiyo, majina yao hayawezi kutajwa.
MAZISHI KUFANYIKA LEO
Alisema ulinzi umeimarishwa katika kanisa lilikotokea mlipuko ili kuhakikisha hakitokei kitu chochote kabla na baada ya mazishi ya watu waliuawa na bomu hilo.
Ibada ya mazishi inatarajiwa kufanyika leo saa 2:00 asubuhi kwenye kanisa hilo na itahudhuriwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na viongozi wa dini mbalimbali, akiwamo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Josephat Lebulu.
Pia ibada hiyo itaanza kwa maandamano kutoka eneo la Burka kwenye makazi ya Askofu Lebulu hadi eneo la Olasiti kanisani na itahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na dini.
HALI ZA WALIOHAMISHIWA MUHIMBILI
Majeruhi saba waliohamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam baada ya kujeruhiwa na mlipuko wa bomu hilo, wameanza kupatiwa matibabu.
Akizungumza na NIPASHE jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Hospitali hiyo, Jeza Waziri, alisema hali za majeruhi, ambao wamelazwa kwenye wodi namba 10 kwenye Jengo la Kibasila zinaendelea vizuri na mara walipowasili walifanyiwa uchunguzi.
“Ni kweli tuliwapokea na mara walipowasili madaktari wetu walianza kuwapatia matibabu, huku wakiangalia jinsi ya kuvitoa vipande vya chuma vilivyopo kwenye miili yao na hali zao kwa ujumla ni nzuri,” alisema Waziri.
Majeruhi hao ni Faustine Shirima, Gabriel Godfrey, Abeid Njau, Jennifer Joaquim, Athanasia Reginald, Fatuma Tarimo na Apolinari Malamsha.
No comments:
Post a Comment