RAIA nane wakiwemo wanne wenye asili ya Kiarabu kutoka nchini
Saudi Arabia na Watanzania wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani
Arusha kwa tuhuma za kuhusika na mlipuko wa bomu lililotokea katika
uzinduzi wa Kanisa la Mtakatifu Joseph, Parokia ya Olasiti mkoani
Arusha, juzi.
Habari ambazo zimezipata kutoka jeshi la polisi mkoani
Arusha, zinadai kati ya Watanznaia wanaoshikiliwa mmoja anatoka Babati
ambaye ndiye anayedhaniwa kurusha bomu hilo.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari, raia hao wa Saudi Arabia
walikamatwa juzi mchana wakiwa njiani kuelekea Namanga mpakani mwa
Tanzania na Kenya.
Inadhaniwa watu hao walikuwa wakitoroka hapa nchini, lakini
walishindwa kufikia azma yao hiyo kutokana na msako mkali wa Jeshi la
Polisi ulioanzishwa baada ya kutokea kwa tukio hilo.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, watuhumiwa hao walihojiwa jana mchana
katika ofisi za makao makuu ya polisi mkoani Arusha ambapo hata hivyo
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabasi, hakuwa tayari
kueleza kile walichokisema.
Wakati huohuo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alikwenda mkoani Arusha
katika eneo la tukio akazungumza waumini kanisani na baadaye kwenda kwa
balozi wa Vatikan hapa nchini na mwakilishi wa Papa Francis, Askofu
Fransisco Padilla.
Waziri Mkuu leo anatarajia kwenda katika Hospitali za KCMC na Mount
Meru kuwajulia hali wagonjwa waliojeruhiwa na mlipuko huo ulioutikisa
mji wa Arusha.
Wakati huohuo viongozi wa dini, serikali na vyama vya siasa nchini
wameungana kutaka utulivu na uvumilivu katika kipindi hiki ambacho taifa
limo katika hali ya sintofahamu kutokana na tukio la kigaidi la
kushambuliwa waumini wa Kanisa Katoliki, mjini Arusha, juzi.
Waumini hao walifikwa na mkasa huo juzi majira ya saa 4 asubuhi wakiwa
katika Misa ya Jubilee ya miaka 50 ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la
Arusha.
W
akizungumza kwa nyakati tofauti, Rais wa Baraza la Maakofu Tanzania
(TEC) Mhashamu askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Sheikh wa BAKWATA wa
mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salim, wamewataka Wakristo na Waislam
kuwa watulivu na kuviacha vyombo vya usalama vifanye kazi ya kuchunguza
wahusika wa tukio hilo.
Wakati viongozi wa dini nchini wakionyesha mshikamano huo, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete jana alikatiza ziara
yake ya kiserikali nchini Kuwait na kurejea nyumbani kuungana na
viongozi wenzake wa serikali na dini kushughulikia tukio hilo.
Akitoa taarifa ya Rais Kikwete kukatiza ziara yake, Mkurugenzi wa
Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, alisema kuwa Rais Kikwete
alitarajiwa kurejea nyumbani leo, lakini alilazimika kukatiza ziara hiyo
na kurejea nyumbani mara moja kuwa karibu na wafiwa pamoja na wale
waliojeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili ofisini kwake
mjini Iringa, Askofu Ngalalekumtwa, alisema kwamba ni utamaduni wa
Wakristo wote duniani kuzidisha sala na maombi wakati wanaposhambuliwa
na kudhuriwa ili atoe jibu kwa wanaohusika na vitendo hivyo.
“Kasi ya sala iendelee ili Mungu wetu wa Amani ajenge fikira za upendo
na haki katika mioyo yetu, sala ndiyo silaha yetu pekee na tunaamini
Mungu atatujibu kwa kuwafichua watu waliohusika na vitendo hivi vya
kihalifu,” alisema askofu Ngalalekumtwa.
Aliwataka waumini kuwa watulivu na kutokata tamaa kuomba kwani Mungu
ndiye mwenye jibu na atatoa majibu kadiri atakavyo kwa wale wote
wanaowatesa wenzao kwa sababu zao binafsi.
“Tulieni na kufanya tafakuri kisha mwambieni Mungu hayo yote ayafanyie
kazi kwa uweza wake. Sisi binadamu tunategemea nguvu kutoka kwake,”
alisema na kuongeza: “Waliopoteza maisha wapokee Rehema ya Mungu na
waliojeruhiwa wafarijiwe na uwezo wa Mungu,” alisema.
Alisema kuwa wakati huu ni wa kutafakari na kumkabidhi Mungu yale yote
yanayowasumbua wanadamu na kuongeza nguvu ya sala ili majibu ya Mungu
yapatikane kwao.
Kwa upande wake Sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salim
amewataka Watanzania kuwa watulivu na wavumilivu na kujizuia kutuhumiana
au kutoa matamshi yenye kuchochea mgawanyiko wa kidini baina yao,
wakati huu vyombo vya usalama vinapoendelea na uchunguzi wa tukio hilo
la kigaidi.
“Kwanza kabisa nawapa pole waliofiwa na ndugu zao katika shambulizi
hilo, na ninawatakia kheri ya kupona haraka wale wote waliojeruhiwa.
Pili ninawaomba Watanzania kuwa watulivu na wavumilivu wakati huu vyombo
vya usalama vinapofanya uchunguzi wa wahusika wa shambulizi hilo,
tusianze kunyosheana vidole na kutoleana kauli za kufarakana kidini,”
alisema Salim.
Naye mwenyekiti wa taasisi ya Imam Bukhary ya jijini Dar es Salaam,
Sheikh Khalifa Khamis, ameitaka serikali kuyadhibiti haraka makundi ya
Waislam yanayoeneza chuki na kuhamasisha kuua watu, kuchoma nyumba za
ibada za dini zingine ili kulinda na kudumisha utulivu na amani ya nchi.
Alitaka viongozi wa dini, hasa wa Kiislam kutokubali dini yao kutumika
na vikundi hivyo kama anuani ya kufanya maovu na kwamba wapaze sauti na
kukana maovu hayo kwamba hayahusiani na imani ya Kiislam.
Alisema kuwa ni wakati muafaka sasa kwa masheikh kutumia njia
zinazowezekana ili kuwafahamisha Waislam katika misikiti yao, mikutano
mbalimbali ya hadhara na katika shughuli za kidini kwamba ni lazima
kufuata mfumo wa Uislam unaokataza maovu.
Alisisitiza kuwa mafundisho ya dini, yanasisitiza amani, upendo baina
ya watu wote, na ndio utamaduni ulioenziwa tangu zamani, hivyo si sahihi
kutumia mgongo wa dini kufanya mambo yanayokwenda kinyume na sheria.
Sheikh Khalifa alinaani kitendo cha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia
yaliyofanywa na magaidi mjini Arusha na kuongeza kuwa vitendo hivyo ni
ukiukwaji wa haki za binadamu.
Aidha kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) Freeman Mbowe ametuma salaam za pole na rambirambi kwa waumini
wa Kanisa Katoliki nchini na Watanzania wote kwa ujumla kutokana na
shambulizi hilo lililotokea katika Kanisa la Olasiti, jijini Arusha,
lililosababisha vifo na majeruhi, huku wengine wakipatwa na mshtuko
mkubwa kutokana na tukio hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya ofisa habari wa CHADEMA, Tumaini Makene, kwa
vyombo vya habari, Mbowe alitoa salaam hizo alipozungumza kwa njia ya
simu na Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padri Antony
Makundi, juzi Jumapili jioni, baada ya kupata taarifa za tukio hilo la
kigaidi.
Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni (KUB)
aliwataka Watanzania wote kuwa watulivu wakati huu, ambapo serikali
kupitia vyombo vya dola inafanya uchunguzi wa tukio hilo.
Aliitaka serikali kuchunguza na kutoa taarifa haraka kuhusu tukio hilo
na matukio mengine yote ya namna hiyo ili kuwapatia Watanzania
matumaini ya kuendelea kuishi kwa utulivu na amani katika nchi yao.
Baadhi ya wakazi wa kawaida wa jiji la Dar es Salaam wamelitupia
lawama Jeshi la Polisi nchini kuwa ndio chanzo cha mashambulizi ya
Arusha kutokana kushindwa kuwakamata baadhi ya watu tangu kuibuka kwa
vitenodo hivyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima jijni Dar es Salaam
jana, kuhusu tukio la kushambuliwa watu waliokuwa kanisani juzi, wakazi
hao walisema kama jeshi hilo halitakuwa makini huenda vitendo hivyo
vikazidi kuendelea nchini.
Walisema kuna matukio ya kushambuliwa viongozi wa kidini, mgogoro
kuhusu kuchinja na kutekwa na kuteswa kwa baadhi ya watu kutokana na
mazingira ya kazi zao hata hivyo, hadi leo hakuna aliyekwishakamatwa
kuhusiana na matukio hayo.
Mmoja wa wakazi hao Mushi Shayo, alisema huu si wakati wa kunyoosheana
vidole bali wanaopaswa kulaumiwa ni jeshi la polisi kutokana na
kushindwa kwao kuwabaini watu hao wanaoleta chokochoko za kigaidi.
Alisema kutowataja watu waliohusika na matukio mbalimbali ndiko
kunakochangia baadhi ya watu hao wabaya kuendelea kufanya vitendo vyao
hivyo.
Naye mwanaharakati, Amos Joseph, alisema umefika wakati kwa Watanzania
kuacha kushabikia mambo bila kujua matokeo yake kwani wataipeleka nchi
pabaya.
Alisema kuna watu hivi sasa wamekwishayapa muelekeo mashambulizi hayo
kuwa yalifanywa na watu wa upande fulani kitendo ambacho kinazidi
kujenga uhusiano mbaya katika jamii.
Tayari jeshi la polisi nchini limesema kuwa linawashikilia watu wanane
kwa tuhuma za kuhusika na mlipuko huo, wanne kati yao ni raia wa Saudi
Arabia na wengine ni Watanzania.
Mlipuko huo ulitokea katika kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph
Parokia ya Olasiti Arusha mjini, juzi Jumapili, na kusababisha vifo
vya watu wawili na kujeruhi 70.
No comments:
Post a Comment