SERIKALI wilayani Kyela kupitia Idara ya Elimu imetangaza
kuifunga Shule ya Msingi Kilasilo iliyopo Kata ya Ikimba kutokana na
kukithiri kwa vitendo vinavyodhaniwa kuwa vya kishirikina
vinavyosababisha shule hiyo pamoja na nyumba za walimu kuwaka moto wa
ajabu wakati wa usiku.
Chanzo cha habari kilifika katika shule hiyo na kuzungumza na viongozi wa
vijiji akiwamo Mwenyekiti wa Kijji cha Kilasilo, Fillipo Mwambela,
ambaye alidai chanzo cha tatizo hilo ni baada ya kuletwa walimu tisa wa
mazoezi shuleni hapo wakitokea Chuo cha Ualimu Mpuguso, wilayani Rungwe.
Alisema baada ya walimu hao kufika, serikali ya kijiji kwa
kushilikiana na uongozi wa shule walitoa jengo moja jipya lililojengwa
kwa nguvu za wananchi lenye vyumba vitatu kwa lengo la kukaliwa na
walimu hao na wengine ambao hawajaripoti.
Baada ya walimu hao kukabidhiwa jengo hilo na kupata kadhia hiyo
wakati wa usiku, walitoa taarifa kwa uongozi wa shule na baadaye
serikali ya kijiji ambayo iliitisha mkutano wa dharura na wazee wa
kimila walikemea na kudai kuwa kama tatizo hilo litaendelea tena
watamtaja anayefanya mambo hayo.
Aliendelea kusema usiku wa siku hiyo mambo yalizidi kuwa makubwa, hali
iliyowalazimu walimu hao kuikimbia na kwenda kuomba hifadhi nyumba za
jirani.
Kaimu Ofisa Elimu Msingi wa Wilaya, Kassim Mtili, mbali na kukiri
kuwepo kwa tatizo hilo pia aliwataka wananchi kuacha kujihusisha na
vitendo vya kishirikina na badala yake wajikite kuwekeza katika elimu
kwa kuwasomesha watoto wao.
Alisema tatizo hilo si la kwanza, kwani katika siku za hivi karibuni
kulikuwapo na tatizo la wanafunzi kuanguka na kupoteza fahamu.
No comments:
Post a Comment