NAIBU Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki, amewataka
wanawake nchini wasiwe ngazi ya wanasiasa kufanikisha mambo yao bali
watumie wingi wao katika kuhakikisha agenda za kuwakomboa zinafanimkiwa.
Kairuki alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua Ilani ya wanawake wa
Tanzania katika Katiba mpya, uzinduzi uliofanyika Mabibo jijini Dar es
Salaam, katika viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
Alisema ingawa sensa iliyofanyika mwaka jana inaonesha wanawake ni
asilimia 51 ya Watanzania wote bado nafasi yao ya kumiliki uchumi wa
nchi hailingani na wingi wao huku katika nafasi za uamuzi wakiwa
hawafiki katika asilimia hizo.
Kutokana na hali hiyo, Kairuki aliwakumbusha TGNP kuwa kazi iliyo
mbele yao kuwakomboa wanawake ni kubwa kuliko mafanikio yaliyopatikana
katika miaka yote ya harakati za ukombozi wa mwanamke katika Tanzania.
“Ninyi TGNP mmefanya uamuzi wa makusudi wa kuwaunganisha wanawake
nchini kuwa na agenda ya sauti moja bila kujali itikadi na tofauti zao
katika kutengeneza Katiba mpya,
Katiba ya nchi ni nyenzo muhimu sana
katika kurekebisha dosari za kihistoria zilizowanyima wanawake fursa
sawa katika nchi,” alisema Kairuki.
Alisema umoja wa wanawake katika kupigania haki yao itawafanya waingie
katika ngazi za uongozi itawaondolea minyororo ya kutokumiliki mali na
itawawekea ulinzi dhidi ya mila na sheria kandamizi dhidi ya ustawi wao.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Ussu Mallya, alisema madai ya
wanawake katika Katiba mpya yanatokana na mawazo ya makundi mbali mbali
yaliyopata fursa kushiriki semina za kila Jumatano inayoendeshwa na
mtandao huo.
No comments:
Post a Comment