Baada ya Mhe. AESHI HILLAL Mbunge wa Sumbawanga Mjini(CCM) kurejeshewa ubunge wake mahakamani,jana tena Mahakama ya Rufaa imemrudishia Ubunge DK. DALALY PETER KAFUMU ambaye alikuwa ni mbuge wa Igunga kwa tiketu ya Chama Cha Mapinduzi -CCM.
Awali, ushindi wa Dk Kafumu (kura 26,428 kati ya kura zote 53,672) ulitenguliwa baada ya mgombea wa CHADEMA, Mwl Joseph Kashindye (aliyepata kura 23,260) kupinga matokeo ya uchaguzi mdogo uliofanyika Oktoba mwaka 2011 akidai ulikuwepo ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.
Kabla ya Kafumu, Igunga ilikuwa chini ya Mbunge, Rostam Aziz (CCM) ambaye alijiuzulu nyadhifa zake za uongozi wa chama na Serikali mwezi Julai mwaka 2011.
Mwezi uliopita, Mahakama ya Rufaa iliketi na kukamilisha kusikiliza rufaa ya kesi hiyo iliyokuwa imefunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ikipinga uamuzi uliomnyang’anya ushindi Dk Kafumu.
Wakili wa Serikali, Gabriel Malata, katika hoja zake za kutaka uamuzi wa Mahakama Kuu utenguliwe, amedai kuwa jaji aliyesikiliza kesi hiyo, alikosea kuanza kuisikiliza kwa kuwa mlalamikaji hakutimiza matakwa ya kisheria.
Malata alidai kuwa mlalamikaji hakulipa ada ya Mahakama Shilingi milioni moja alizotakiwa kutoa au hati ya nyumba, kabla kesi hiyo haijaanza kusikilizwa kama Sheria ya Uchaguzi inavyoelekeza.
Aliendelea kudai kuwa mjibu rufaa, aliyekuwa mgombea wa ubunge kwa tiketi ya Chadema katika uchaguzi huo, Joseph Kashindye, na wenzake hakutekeleza sharti hilo na hivyo usikilizwaji wa shauri hilo, pamoja na mwenendo mzima wa kesi ni batili.
Wakili huyo amedai kwamba malalamiko yaliyopelekwa Mahakama Kuu ni ya kutengeneza, kwani hayajawahi kuwasilishwa katika Kamati ya Maadili ya Uchaguzi, kama ilivyofanyika katika suala la Mbunge wa Tabora mjini, Ismali Aden Rage, ambaye alitozwa faini ya Sh laki moja kwa kutembea na silaha kwenye mkutano.
Hoja hizo zilipingwa na wakili wa Kashindye, Profesa Abdalah Safari, ambaye aliitaka Mahakama ya Rufaa, kutupilia mbali hoja hizo. Profesa Safari alidai kwamba Mahakama Kuu iliyosikiliza kesi hiyo, iliridhika kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria wakati wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga, ndipo ikaridhia kutengua matokeo.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa chini ya uenyekiti wa Jaji Nathalia Kimaro, akisaidiana na Jaji William Mandia na Jaji Semistrocles Kaijage, baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, waliahidi kutoa uamuzi wao mara baada ya kupitia kwa undani mwenendo mzima wa shauri hilo.
Mahakama Kuu ya Tanzania ilitengua matokeo ya uchaguzi huo, baada ya kubainika kuwa uchaguzi huo ulitawaliwa na vitendo vya rushwa, kampeni chafu na vitisho dhidi ya wapiga kura.
Jaji Mary Nsimbo Shangali wa Mahakama Kuu, alitangaza kutengua matokeo hayo, baada ya mahakama hiyo kuridhika na hoja saba zilizowasilishwa na upande wa mlalamikaji kati ya hoja 17 zilizowasilishwa katika mahakama hiyo. .
No comments:
Post a Comment