KUTOKANA na ongezeko la kodi katika huduma za simu za mkononi, gharama za huduma hizo zitaongezeka kuanzia Julai mosi mwaka huu.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana na Umoja wa
wenye makampuni ya simu za mkononi Tanzania (MOAT) imesema pendekezo la
serikali la kuweka kodi ya asilimia 14.5 kwenye huduma za simu za
mkononi linalazimu kupanda kwa gharama.
MOAT imesema awali kodi ilikuwa ikitozwa asilimia 12.5 katika huduma
ya mawasiliano ya simu na kwamba ongezeko la kufikia asilimia 14.5
tofauti na nchi za jirani Kenya na Uganda ambazo zimeendelea kutoza
viwango vya ushuru vya asilimia 10 huku wakilalama asilimia 12.5, ni
mzigo kwa watumiaji wa huduma zao.
“Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2013 unaainisha kuwa huduma za
mawasiliano ni huduma yoyote ya maelezo inayotolewa na makampuni ya
mawasiliano ya simu kwa njia ya mawasiliano.
“Kwa kutoa au kupokea sauti, maandishi, picha au taarifa kupitia mfumo
wa kielektroniki.” Ilieleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na
Vodacom, Airtel, Tigo na Zantel.
MOAT ilieleza kuwa eneo mojawapo litakaloathirika ni huduma za
intaneti ambalo linahitaji kuwekewa mikakati ya kulikuza kutokana na
umuhimu wake katika maisha ya sasa kiuchumi na kijamii.
“Hatua hii ya kuongeza kodi itakwenda kinyume na mipango iliyopo yenye
lengo la kuibadili jamii kwa kuipatia maarifa ya msingi kupitia huduma
ya intaneti na mawasiliano ya simu,” taarifa ilisema.
Kwa mujibu wa MOAT, Tanzania ni kati ya nchi zenye kiwango cha chini
ya matumizi ya huduma ya mtandao wa intaneti barani Afrika, ambapo
watumiaji wa huduma hiyo ni asilimia 10, ikilinganishwa na Kenya yenye
watumiaji asilimia 40.
“Hivi sasa, upanuzi wa mawasiliano na miundombinu vijijini ndiyo
kipaumbele cha sekta nzima. Tunaamini hapa ndipo ukuaji wa sekta ya
mawasiliano ya simu itakapoonekana katika miaka ijayo,” ilifafanua
taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment