MWANAKIJIJI wa Ihanda, John Mjwanga (36), amehukumiwa kifungo
cha miaka 25 jela kwa kosa la kumuuza mtoto wake wa kiume wa miaka 10
kwa sh milioni 1.1 ili akachunwe ngozi.
Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Mahakama ya Wilaya ya Kyela, mkoani
Mbeya na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Joseph Luambano, aliyedai kuridhishwa na
ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri.
Mbele ya hakimu huyo, Mwendesha Mashitaka, Nicholaus Tiba, alidai
kwamba Novemba 17 mwaka 2010 mtuhumiwa huyo alikwenda Kasumulu kwenye
mpaka wa Wilaya ya Kyela na Mbozi kutafuta wateja wa ngozi ya binadamu.
Ilidaiwa kwamba akiwa huko mtuhumiwa alikutana na Israel Edgar ambaye
ni mfanyabiashara wa kuuza na kununua fedha za kigeni, hivyo
walikubaliana.
Mwendesha Mashitaka, Tiba, alidai kwamba baada ya makubaliano
mfanyabiashara huyo alitoa taarafa kituo cha polisi ambapo mkuu wa
upelelezi alifika eneo hilo akijifanya mteja.
Kwa mujibu wa mwendesha mashitaka huyo, mtuhumiwa bila kujua
alikubaliana bei na mkuu wa upelelezi kisha alikwenda kumchukua mtoto
wake na kurejea kesho yake.
Ushahidi uliotolewa mahakamani ulidai kwamba mtuhumiwa alimchukua
mtoto wake akimdanganya kuwa anampeleka kwa shangazi yake ili akasome
ndipo alipompigia simu mkuu wa upelelezi aandae malipo.
Ushahidi huo ambao haukutiliwa shaka na mahakama, uliendelea kudai
kwamba walikubaliana wakutane Kasumulu Motel, eneo ambalo askari polisi
waliweka mtego uliofanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ambaye
alikabidhiwa sh 200,000 na kukamatwa.
No comments:
Post a Comment