Juzi, Jiji la Arusha na vitongoji vyake lilikumbwa na taharuki
nyingine wakati polisi waliporusha mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi
wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema), ambao walikuwa
wamekusanyika kwenye Uwanja wa Soweto.
Inakaribia wiki moja sasa Jiji la Arusha na
vitongoji vyake limekuwa katika hali tete. Watu wanashindwa kwenda
kazini na kufanya shughuli zao za kila siku.
Ikumbukwe kwamba katika tukio la Jumamosi, watu walikufa na wengine kadhaa kujeruhiwa miongoni mwao vibaya kiasi kwamba bado wanauguza majereha makubwa waliyoyapata kutokana na tukio hilo. Kimsingi, bado Arusha inaomboleza vifo vya waliopoteza maisha katika tukio hilo, pia wengine wanaugulia machungu na majeraha waliyoyapata. Ni kwa bahati mbaya kwamba wapo ambao wameshindwa kutambua hili na kuendelea kuliweka jiji hili njiapanda.
Ni kama kuna mashindano yasiyo rasmi kati ya Chadema na wafuasi wao kwa upande mmoja na polisi na Serikali kwa upande mwingine. Mashindano ambayo hayana tija kwani yanaiweka Arusha na watu wake katika wakati mgumu.
Swali la kujiuliza ni kwamba hivi kinachotokea hivi sasa katika mji huu ni kwa faida ya nani? Ni dhahiri kwamba jibu la swali hili ni jepesi tu. Si Serikali, Chadema wala polisi wanaonufaika na hali tete ya Arusha.
Tunapoteza muda ambao ungetumika kufanya mambo mengine muhimu ya nchi na zaidi ya yote, matukio haya yanaathiri uchumi wa Mkoa wa Arusha kwa kiasi kikubwa na watu wake kwa jumla. Athari hiyo hakuna ubishi kwamba inaligusa taifa moja kwa moja kutokana na uenyeji wa mkoa huo katika sekta ya utalii.
Tunasema hivi tukirejea kuwapo kwa taarifa kwamba makundi ya watalii waliokuwapo Arusha yalianza kuondoka kwenda Moshi na Dar es Salaam kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama.
Baadhi yao wameripotiwa kusitisha au kufuta kabisa
safari zao za utalii kutokana na hali hii. Haya ni matokeo ya sasa,
lakini athari zinaweza kuwa kubwa zaidi ikiwa hali ya usalama
haitadhibitiwa.
Hivi kuna tulilojiuliza juu ya hili na kutafakari kwa kina athari zake? Tujiulize swali dogo tu, hao wanaoelezwa kwamba wamekatisha ziara au kuondoka, watakwenda kusema nini huko kwao? Tukumbuke usemi wa wahenga, ubaya unavuma kuliko wema.
Busara kubwa inahitajika kwa pande zote husika ili
kuirejesha Arusha katika hali ya kawaida. Ubabe na matumizi ya silaha
na aina nyingine ya vurugu kamwe haviwezi kuwa suluhisho la matatizo
yaliyopo.
Serikali inapaswa kuhakikisha kwamba wananchi wa Arusha na mali zao wanakuwa salama na kuhakikisha kwamba watalii na wageni wengine ambao wanafika katika mji huo kwa wingi, wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
Kama tulivyosema katika tahariri yetu jana, tayari polisi wametuhumiwa kwamba nao wanahusika katika matatizo yaliyopo.
Ni wajibu na jukumu la jeshi hilo hasa likizingatia kaulimbiu yake ya polisi jamii, kuhakikisha kwamba linarejesha imani yake kwa wananchi wa Arusha na kujaribu kuepuka kwa namna yoyote ile kuonekana kwamba jeshi hilo lililoapa kuwalinda wananchi na mali zao linawanyanyasa.
Ni wajibu na jukumu la jeshi hilo hasa likizingatia kaulimbiu yake ya polisi jamii, kuhakikisha kwamba linarejesha imani yake kwa wananchi wa Arusha na kujaribu kuepuka kwa namna yoyote ile kuonekana kwamba jeshi hilo lililoapa kuwalinda wananchi na mali zao linawanyanyasa.
No comments:
Post a Comment