NAIBU Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba, leo
anatarajia kuwa mgeni rasmi katika shindano la kumsaka malkia wa Redd’s
Miss Tanga, linalotimua vumbi katika Uwanja wa Mkwakwani mkoani hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Mkurugenzi wa
DATK Entertainment inayoandaa kinyang’anyiro hicho, Asha Kigundula,
alisema maandalizi yamekamilika, kilichosalia ni muda kufika na mrembo
kuwekwa hadharani.
Kwa mujibu wa Kigundula, Redd’s, Miss Tanga, inadhaminiwa na L Hayat
Investment Limited, Dodoma Wine, CXC Africa, Executive Solutions, Busta
General Supply, Mkwabi Enterprises, Lusindic Investment LTD na Lavida
Pub.
Wadhamini wengine wa kinyang’anyiro hicho ni pamoja na Jambo Leo, Staa
Spoti, Five Brothers, Clouds Media, pamoja na magazeti tando (blogs) za
Michuzi Media Group, Bongostaz.com, Saluti5, Kajuna, JaneJohn, Kidevu
na assengaoscar.blogspot.com.
“Nashukuru Mungu mambo yameenda sawa, kilichokuwa kimebaki ni
kumtangaza mgeni rasmi na tumeshampata tayari, ambaye ni Mbunge wa
Bumbuli, Mheshimiwa Makamba. Tuzidi kuomba Mungu atuongoze katika
mchakato mzima kesho ili mambo yaende sawa,” alisema Kigundula.
Aidha, Kigundula alisema DATK imeamua kutoa zawadi ya fedha taslimu
kwa washindi na si vitu, ili warembo wake waweze kupata fursa ya
kujiamulia manunuzi wao wenyewe kuliko kununuliwa, ambapo alisema
mshindi wa kwanza atajishindia shilingi 500,000, wa pili 300,000 na wa
tatu 250,000.
Mshindi wa nne na tano watapata shilingi 200,000 kila mmoja na warembo
wengine watakaosalia watapata kifuta jasho cha shilingi 100,000 kila
mmoja, huku akifichua uwapo wa zawadi maalumu kwa mrembo mwenye nidhamu
ili kuliboresha shindano hilo.
Kigundula alisema, kwa upande wa burudani, msanii wa kizazi kipya,
Khaleed Tunda ‘Tunda Man,’ ataongoza safu ya burudani, ambayo itakuwa na
wasanii mbalimbali wakiwamo Dk. John, Nabisha kutoka kundi la THT, Fady
Dady na wasanii chipukizi kutoka mkoani hapa.
Kigundula alisema shindano hilo linatarajiwa kuanza majira ya saa
mbili usiku na kushirikisha warembo 12 ambao watachuana ili kuweza
kumpata malkia wa mkoa huu ambaye atauwakilisha katika mashindano hayo
ngazi ya Kanda kuelekea Redd’s Miss Tanzania.
Warembo hao ni Hawa Ramadhani (18), Hazina Mbaga (19), Like Abdulraman
(19), Irene Thomas (20), Tatu Athumani (19), Winfrida Gutram (21), Lulu
Mbonela (19), Hazina Daniel (19), Lulu Matawalo (22), Judithi Moleli
(21), Neema Jonas na Hawa Twaybu (21).
Aliongeza kuwataka wakazi wa Tanga na mikoa ya jirani kujitokeza kwa
wingi kushuhudia shindano hilo la aina yake ambalo litajenga historia
mpya kwa mkoa huu.
No comments:
Post a Comment