TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imefungwa mabao 4-2 dhidi ya Ivory Coast na kuzima harakati zake za kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014 huko Brazil.
Watanzania
wengi na wadau wa michezo walidhani Taifa Stars ingeweza kusonga mbele katika
harakati hizo za kufuzu kucheza Kombe la Dunia 2014, lakini sasa ukweli
umejidhihirisha.
Sasa
wengi wamekubaliana na uhalisia wa mambo kwamba, inahitaji muda kidogo kuona
Taifa Stars ikisonga mbele katika kuelekea kufuzu Kombe la Dunia na siyo rahisi
kama ilivyodhaniwa hapo kabla.
Ni
mambo mengi yaliyotokea katika mchezo dhidi ya Ivory Coast ambayo yaliigharimu
Taifa Stars licha ya uwanja kujaa idadi kubwa ya mashabiki waliokuwa
wakiishangilia timu yao bila kuchoka.
Jambo
la msingi ni kwamba, Taifa Stars ikiwa katika harakati za kuhakikisha inafuzu
Kombe la Dunia wengi tulisahau kwamba, kwa ‘reality’ ilikuwa ngumu kwa Taifa
Stars kufuzu fainali hizo japokuwa kwa mapenzi tulidhani timu hii ingeweza
kufuzu kwa kuanza na vipigo kwa timu za Morocco na Ivory Coast.
Tukitazama
mchezo kati ya Taifa Stars na Ivory Coast kuna baadhi ya mambo yalionekana
kwamba bado tuna safari ndefu ya kufuzu Kombe la Dunia kama kweli tuna nia ya
kufanya hivyo.
Mambo
mengi mno yalijitokeza katika mchezo kati ya Taifa Stars dhidi ya Ivory Coast
na haya ni machache kati ya mengi yake;
TAIFA
STARS ILICHEZA KUFURAHISHA MASHABIKI SIYO KUIFUNGA IVORY COAST
Kiungo
wa Manchester City, Yaya Toure alicheza kama mshambuliaji na alitimiza majukumu
yake kama straika hasa kwa kutokubali kukaa na mpira kwa muda mrefu licha ya
kuwa na uwezo wa kufanya hivyo.
Wakati
Toure mwenye uwezo wa kumiliki mpira atakavyo na kufanya jambo lolote hakutoa
nafasi hiyo zaidi ya kutafuta ushindi kwa timu yake, viungo na wachezaji wengi
wa Taifa Stars walikuwa wakitumia muda mwingi kukaa na mpira bila ya sababu ya
msingi.
Kiungo
Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ mara nyingi alikuwa kitumia muda mwingi kukaa na
mpira na kutaka kupambana na wachezaji wa Ivory Coast licha ya kuonekana wazi
kwamba mara zote alizidiwa nguvu.
Tazama
hata Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto na Frank Domayo walikuwa wakitumia muda
mwingi ‘ku-hold’ mipira huku wakitoa pasi zisizo na macho na kujikuta
wakipoteza mipira mingi kutokana tu na vitendo vyao vya kuchelewesha mipira.
Pamoja
na vitendo hivyo kuwa hatari kwa timu, lakini mashabiki walikuwa
wakiwashangilia kwa nguvu viungo wa Taifa Stars bila ya kujua madhara ya
kufanya hivyo. Hao walijali zaidi kushangiliwa kuliko umuhimu wa mchezo husika.
Taifa
Stars ilihitaji zaidi kucheza kwa kutokubali kukaa na mpira kwa muda mrefu kwa
wachezaji wake ili kuitengeneza nafasi za haraka za kupata bao ili iweze
kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Kuanzia
Sure Boy, Kiemba, Kazimoto na Domayo, wote walionekana kufurahishwa na kelele
za mashabiki waliokuwa wakiwashangilia kutokana na chenga na madoido mengine
waliyokuwa wakiyafanya uwanjani.
SAFU
YA ULINZI ILIPAPARIKA
Ilikuwa
kama kila mchezaji ameahidiwa kiasi kikubwa cha fedha, kwani mara nyingi
wachezaji wa Taifa Stars hawakucheza katika nafasi zao na hilo liligharimu timu
na kujikuta wakilala mabao 4-2.
Erasto
Nyoni ndiye beki anayeweza kuondoka na lawama nyingi lakini halikuwa kosa lake
wakati mwingine kwani alilazimika kwenda katikati kusahihisha makosa ya mabeki
wa kati na kuisahau nafasi yake.
Ilionekana
wazi kwamba yalikuwepo mawasiliano hafifu juu ya kutengeneza mtego wa kuotea
yaani ‘offside trick’ na matokeo yake Ivory Coast walitumia vyema mwanya huo na
kujipatia mabao manne.
Baada
ya kuonekana ‘njia’ tangu dakika za mwanzo, beki Erasto Nyoni inaonekana
hakupata ushauri wa kutosha kuhusu kutulia na kucheza soka kwani hata makelele
ya mashabiki yalimfanya aonekane mtu asiyefaa kikosini. Lakini alikuwepo benchi
anayeweza kumudu nafasi yake moja kwa moja?
NGUVU
HAFIFU
Wachezaji
wengi wa Taifa Stars walionekana kutokuwa na nguvu ya kupambana na wenzao wa
Ivory Coast kutokana na hali halisi ya miili yao.
Sure
Boy mfupi na mwenye mwili mdogo alionekana kama mchezaji wa kawaida mbele ya
Yaya Toure mwenye mwili mkubwa na nguvu, na mara nyingi Toure aliiwahi mipira
ambayo ingeweza kuwahiwa na Sure Boy.
Domayo
naye hakuweza kufua dafu mbele ya Traore Lucina na Jean Jacques ambao wote ni
watu wa miraba minne.
WAO
WALIMKATAA KALOU, SISI TUKAFUATA SAMBUSA
Kabla
hata ya mapumziko, waandishi kadhaa wa Ivory Coast walionekana kutopendezwa na
uchezaji wa Salomon Kalou ambaye muda mwingi kila alipopewa mpira alikuwa
akitaka kukaa nao kwa muda mrefu kama ilivyokuwa kwa kina Sure Boy na wengine
wa Taifa Stars.
Waandishi
hao walionekana wazi kuchukizwa na hali hiyo na mara kwa mara walionyesha wazi
kutoridhika na uchezaji wa Kalou.
Ulipofika
wakati wa mapumziko, waandishi hao walishuka chini katika vyumba vya
kubadilishia na kuzungumza na baadhi ya maafisa wa timu yao ili kutazama
uwezekano wa kumpumzisha Kalou kwa maslahi ya nchi.
Wakati
hayo yakitokea kwa Ivory Coast, waandishi wa Tanzania walikuwa wamekaribishwa
ukumbi wa VIP kupata vitafunwa kama sambusa, mishikaki na vinywaji baridi, hao
hawakuwaza kupeleka mawazo yao kwa benchi la ufundi na hata wangefanya hivyo
wasingesikilizwa kutokana na utaratibu ulivyo.
Mbaya
zaidi siyo waandishi tu, hata viongozi kadhaa wa Kamati ya Ushindi ya Taifa
Stars nao walionekana wakiwa VIP wakijichana kana kwamba Taifa Stars ipo katika
nafai nzuri. Kumbuka hadi muda huo timu ilikuwa ipo nyuma kwa mabao 3-2.
HONGERA
ULIMWENGU
Kama
kuna mchezaji wa Ivory Coast aliyeomba mpira uishe haraka kuliko wengine basi
ni Bamba Souleman ambaye alikuwa akicheza kama beki wa kati anayemkaba
mshambuliaji wa Taifa Stars, Thomas Ulimwengu.
Ulimwengu
alimmudu vizuri Bamba kiasi cha kumkimbiza na kuufanya mpira atakavyo hadi
kufunga bao moja. Mara nyingi Bamba alizidiwa nguvu na kasi na Ulimwengu kiasi
cha kulalamikiwa na wenzake.
Kama
wachezaji wanne tu wa Taifa Stars wangeweza kucheza kama Ulimwengu, ni wazi
timu hiyo ingepata matokeo mazuri na ya kuridhisha.
BY ELIUS KAMBILI
No comments:
Post a Comment