VIDEO za nyimbo za Injili za kwaya za madhehebu ya dini hapa
nchini, zinapaswa kubeba taswira halisi ya imani na matendo ya
Kikristo, badala ya matukio ya burudani, starehe na kuiga mifumo ya
Kimagharibi.
Hayo yalisemwa na Tully Msyani, aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi
wa harambee ya kuchangia gharama za kutayarisha filamu ya uinjilishaji
iliyoandaliwa na kwaya ya vijana wa Kanisa la Wasabato, Mbeya Mjini.
Msyani alisema kuwa nyimbo za Injili zimekuwa zikiwavutia watu wengi
hasa waumini, lakini anashtushwa na namna zinavyoandaliwa, kutumia
gharama kubwa na watu kusafiri kwenda mbali, wakati kile
kinachokusudiwa kuonekana hakiendani na ujumbe wa nyimbo zinazoimbwa.
Alisema kuwa ipo haja vijana wa kanisa hilo wakabadili mfumo wao wa
kutengeneza video zao kwa kukwepa gharama na maeneo yasiyokuwa muhimu
katika utengenezaji wake, ili kazi zao ziweze kuuzwa kwa bei nafuu na
watu wengi waweze kumudu kununua.
“Tumekuwa na tabia ya kuigana sana, lazima kazi zenu ziwe ‘unique’.
Huwezi kuimba wimbo wa mateso ya Yesu huku video inaonyesha majengo ya
ghorofa ya Arusha au mpo barabarani huku magari ya kifahari yakipita,
sidhani kama watu wanajua wanachotakiwa kukifanya,” alisema Msyani.
Alisema kuwa nyimbo za injili zinapaswa kuwagusa na kuwabadilisha
watu wanaozisikiliza ili waendane na matendo mema badala ya kuwafanya
wengi wacheze na kuzifurahia bila kusikiliza ujumbe uliopo, na kwamba
sehemu kubwa inapaswa kuwa ya kuwajenga watu kiimani.
Aidha, Mchungaji wa Kanisa la Wasabato Mbeya Mjini, Steven Ngusa
aliwapongeza vijana wa kanisa hilo kwa kuwa wabunifu na kwamba kiasi
cha zaidi ya sh milioni 10 wanazohitaji kwa ajili ya kuandaa filamu yao
zitachangwa na waumini wote wenye mioyo safi.
Mwenyekiti wa Vijana wa Kanisa hilo, Nyanswi Mwita alisema kiasi cha
sh milioni 4.7 kilitolewa na waumini wa kanisa hilo na wageni
mbalimbali walioalikwa ili kuweza kuchangia fedha za kutengeneza video
hiyo, huku akiahidi kutekeleza ushauri uliotolewa na mgeni rasmi.
No comments:
Post a Comment