CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema Muungano wa
serikali mbili za sasa unatumia gharama kubwa kuliko serikali tatu
zinazopendekezwa karika rasimu ya Katiba Mpya.
Kimesema hoja ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kupinga shirikisho la
serikali tatu kwa kigezo cha ukubwa wa gharama ni potofu kwa sababu
mfumo unaopendekezwa utapunguza utitiri wa vyeo na kudhibiti matumizi
yasiyo ya lazima.
Tanzania Daima imeona andishi la CHADEMA linalotarajiwa kuzinduliwa
wakati wowote kuanzia sasa, ambalo ndiyo msimamo rasmi wa chama hicho
kuhusu rasimu ya Katiba Mpya.
Miongoni mwa mambo mengi yanayochambuliwa kwa vielelezo ni hoja ya
serikali, ambayo CCM imekuwa inahamasisha wanachama wake waikatae, na
badala yake wapendekeze serikali mbili za sasa kwenye mabaraza ya katiba
yanayoendelea.
CHADEMA imesema kuwa madai ya CCM kuwa serikali ni mzigo kwa taifa,
hayana ukweli kwani serikali mbili za sasa zinatafuna mabilioni ya
shilingi ambayo yataokolewa iwapo serikali zitakuwa tatu.
Katika kifungu cha ukubwa wa serikali, CHADEMA imesema kwa muundo wa
sasa wa serikali mbili, kuna viongozi wakuu sita (6), wakati mfumo wa
serikali tatu utakuwa na viongozi wasiozidi wanne (4). Imesema wabunge
na wawakilishi 438, huku katika serikali tatu kutakuwa na wabunge
wasiozidi 314.
Kwamba pamoja na hesabu hii, bado upo uwezekano wa idadi hii kupungua
zaidi kwa kuwa mchakato wa kuandika Katiba ya Tanganyika na
marekebisho/mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar kutokana na mabadiliko ya
muundo wa Muungano unaweza kuja na mifumo tofauti ya uwakilishi au
mgawanyo wa majimbo mapya ya uchaguzi.
“Bunge la Jamhuri ya Muungano la sasa lina idadi ya wabunge 357,
ukitoa wabunge 189 wa majimbo ya uchaguzi ya Tanzania bara na 50 ya
Zanzibar; 102 wa viti maalumu na 10 wa kuteuliwa na rais, watano
wanaowakilisha Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Mwanasheria Mkuu.
“Kwa upande wa Baraza la Wawakilishi kuna jumla ya wawakilishi 81-50
wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi, 10 wa kuteuliwa na Rais wa Zanzibar,
20 wa viti maalumu, na mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, kwa maana hiyo kwa
muundo wa sasa wa Muungano, mabunge mawili tuliyonayo yana idadi ya
wabunge 438.
“Idadi hiyo ni kubwa kuliko idadi ya wabunge wa mabunge matatu
yatakayokuwepo chini ya muundo wa serikali tatu kwa wabunge 124,”
imesema CHADEMA.
Ukweli huu unaiweka pabaya CCM ambao walidai kuwa serikali tatu
inayopendekezwa na tume na kuungwa mkono na wapinzani itakomba fedha
nyingi za Watanzania.
“Mapendekezo ambayo ndiyo msimamo wa chama tulishayawasilisha kwenye
tume kuwa sisi tunapendekeza mfumo wa serikali mbili na siyo tatu wala
moja,” alisema Nape alipokuwa akitoa taarifa ya uamuzi wa Kamati Kuu
(CC) ya CCM iliyokutana usiku wa kuamkia jana kujadili suala hilo.
Kauli ya Nape inafanana na matamshi ambayo yamewahi kutolewa na baadhi
ya wanasiasa wakongwe ambao ni makada wa CCM, wakiwamo mawaziri wakuu
wastaafu, Frederick Sumaye na John Malecela, Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Samuel Sitta na baadhi ya wabunge ambao mara kadhaa
wamekaririwa wakipinga pendekezo la serikali tatu.
Hata hivyo, wabunge wa Zanzibar, akiwemo Mbunge wa Uzini, Mohamedi
Seif Khatibu na Mjumbe wa Kamati ya Halmashauri Kuu ya CCM, Balozi Seif
Idd, walisema watu watakaopinga serikali mbili wafukuzwe Chama Cha
Mapinduzi.
Ifuatayo ni sehemu ya msimamo wa CHADEMA kuhusiana na uendeshaji wa serikali tatu:
Kwanza, hadi sasa hakuna mtu yeyote au taasisi yoyote iliyofanya
uchambuzi wa uangalifu wa gharama za kuendeshea serikali, iwe moja,
mbili au tatu katika nchi yetu. Kwa sababu hiyo, hakuna ushahidi wowote
wa kuthibitisha kwamba kuendesha serikali tatu ni ghali zaidi kuliko
kuendesha serikali mbili.
Pili, Kama suala la gharama za kuendeshea serikali ndio jambo muhimu
zaidi katika kuamua muungo wa Muungano, wanaopinga shirikisho la
serikali tatu wangeeleweka kama wangependekeza muundo wa serikali moja
tu, badala ya serikali mbili za sasa wanazoziunga mkono, au hata tatu
zinazopendekezwa na rasimu.
Tatu, kama mapendekezo ya rasimu juu ya mambo ya Muungano
yakichukuliwa kuwa kigezo cha kupima ukubwa wa serikali na gharama za
kuiendesha, basi gharama za serikali ya Muungano zinaweza kuwa ndogo
sana.
Nne, kama mambo saba ya Muungano yanayopendekezwa na rasimu,
hakutakuwa na zaidi ya wizara nne za Serikali ya Muungano.
Hivyo kwa
mfano kutakuwa na Wizara ya Katiba na Sheria itakayoshughulikia masuala
ya katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano; Wizara ya Ulinzi
itakayokuwa na majukumu ya ulinzi na usalama wa Jamhuri ya Muungano na
Wizara ya Fedha itakayoshughulikia masuala ya sarafu, Benki Kuu na
ushuru wa bidhaa na mapato yatokanayo na mambo ya Muungano, na Wizara ya
Mambo ya Nje.
Masuala yaliyobaki yaani uraia na uhamiaji na usajili wa vyama vya
siasa hayastahili kuwa na wizara zinazojitegemea, kwa hiyo yanaweza
kuwekwa chini ya wizara zilizotajwa.
Aidha aya ya 93(2) ya rasimu inapendekeza ukubwa wa Baraza la Mawaziri
wasiozidi kumi na tano. Hata hivyo aya ya 93(3) inaelekeza kwamba
Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na wizara kwa kuzingatia mamlaka
ya serikali kwa mujibu wa katiba hii, kwa namna nyingine ukubwa wa
serikali lazima uzingatie mambo saba ya Muungano. Kwa sababu hiyo
Serikali ya Jamhuri ya Muungano haiwezi kuwa na mawaziri wengi kuliko
mambo saba ya Muungano.
Kwa mtazamo huo huo, aya 93(3) na orodha ya mambo ya Muungano kama
kipimo cha ukubwa wa Srikali ya Muungano haiwezekani katibu mkuu
kiongozi na makatibu wakuu wanaopendekezwa katika aya za 98 na 99 za
rasimu kuwa zaidi ya wanne.
Kwa kuzingatia idadi ya makatibu wakuu wenyewe, kamati maalumu ya
makatibu wakuu inayoelekezwa katika aya ya 100 na Sekretarieti ya Baraza
la Mawaziri inayotarajiwa katika aya ya 101 hazina maana wala umuhimu
wowote kikatiba.
Kwa kuzingatia mapendekezo ya rasimu kuhusu Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika aya ya 105, kwa idadi ya sasa ya mikoa ya
Tanzania bara na wilaya za Zanzibar, Bunge la Jamhuri ya Muungano
litakuwa na wabunge 75 kwa mapendekezo ya muundo wa serikali tatu,
endapo Bunge la Zanzibar litakuwa na wabunge 50 wa majimbo ya sasa ya
uchaguzi.
Kwa maana hiyo muundo wa Muungano wa serikali tatu utakuwa na mabunge
matatu yenye jumla ya wabunge 314. Upo uwezekano wa idadi hii kupungua
zaidi kwa kuwa mchakato wa kuandika katiba ya Tanganyika na
marekebisho/mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar kutokana na mabadiliko ya
muundo wa Muungano unaweza kuja na mifumo tofauti ya uwakilishi au
mgawanyo wa majimbo mapya ya uchaguzi.
Kwa kulinganisha Bunge la Jamhuri ya Muungano la sasa lina idadi ya
wabunge 357, ukitoa wabunge 189 wa majimbo ya uchaguzi ya Tanzania bara
na 50 ya Zanzibar; 102 wa viti maalumu na 10 wa kuteuliwa na rais,
watano wanaowakilisha Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Mwanasheria
Mkuu.
Kwa upande wa Baraza la Wawakilishi kuna jumla ya wawakilishi 81-50
wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi, 10 wa kuteuliwa na Rais wa Zanzibar,
20 wa viti maalumu, na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, kwa maana hiyo kwa
muundo wa sasa wa Muungano, mabunge mawili tuliyonayo yana idadi ya
wabunge 438. Idadi hiyo ni kubwa kuliko idadi ya wabunge wa mabunge
matatu yatakayokuwepo chini ya muundo wa serikali tatu kwa wabunge 124!
Taasisi nyingine za Muungano zinazopendekezwa kama vile Tume ya
Mahusiano na Uratibu wa Serikali, na Tume ya Utumishi wa Umma haziwezi
kuwa kubwa sana kwa kuzingatia ukubwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano
kwa mujibu wa rasimu.
Taasisi nyingine kama vile Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji,
Tume ya Haki za Binadamu hazipo kwenye orodha ya mambo ya Muungano na
uwepo wao kwenye rasimu unakinzana na matakwa ya aya za 59 na 60 za
rasimu.
Kama majukumu ya taasisi hizo hayahusu mambo ya Muungano, tume haziwezi kugharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Hata hivyo baada ya kukubalika kwa pendekezo la kuyaingiza masulala
hayo katika orodha ya mambo ya Muungano, bado gharama zinaweza
kupunguzwa kwa kuweka mfumo wa utekelezaji wa taasisi husika kupitia
makubaliano na washirika wa Muungano.
Majukumu ya utekelezaji wa mambo mengine ya Muungano kama uchaguzi na
usajili wa vyama vya siasa yanaweza kutekelezwa na taasisi husika za
washirka wa Muungano kwa makubaliano na masharti maalumu chini ya aya ya
59(3) ya rasimu. Hii nayo itapunguza gharama za kuendesha Serikali ya
Jamhuri ya Muungano.
Via Tanzania Daima
Tunakipongeza sana chama cha CHADEMA ambacho siku zote kinasimamia haki za wananchi.Kimsingi CCM haitaki mabadiliko na kuangalia maslahi ya chama badala ya raia.
ReplyDeleteUwepo wa serikali tatu utatatuwa kero nyingi zinazotokana na muundo wa sasa wa muungano.
Isipokuwa kikubwa ni kila nchi (Tanganyika na Zanzibar) kuwa na mamlaka kamili za kiutawala ambapo mambo saba yaliyopendekezwa kwenye rasimu bado haipelekei kila nchi kuwa na mamlaka kamili.Hivyo mambo yote saba yasiwepo katika serikali ya muungano ili kuwepo na fursa kubwa kwa kila nchi kuamua mambo yake yenyewe.Baada ya mchakato wa katiba ya Tanganyika kukamilIka ndipo nchi mbili zikae na kuamua mambo yapi yaIngizwe kwenye katiBa ya muungano.