RAIS Jakaya Kikwete amesema uchochezi wa baadhi ya wanasiasa
kuhusiana na gesi asilia iliyogunduliwa nchini ni changamoto kwa
serikali yake ambayo iko tayari kupambana nayo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam kwa vyombo
vya habari na
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Rais Kikwete
alitoa msimamo huo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati alipokutana na
kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa kundi la kampuni za British Gas
(BG) Chris Finlayson, moja ya kampuni zilizogundua gesi na kuanza
kuwekeza katika uchimbaji wa rasilimali hiyo.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais
Kikwete alimwambia Finlayson na ujumbe wake kuwa gesi asilia hiyo
inayoendelea kugunduliwa nchini ni rasilimali muhimu na lazima itumike
kuwatoa watu katika umaskini na ibadilishe maisha.
“Maandalizi ya uchimbaji wake yasichukue muda mrefu ...miaka 10
hivi….. huu ni muda mrefu sana kwa sababu wananchi wetu wanahitaji kuona
manufaa ya gesi asilia hiyo katika kipindi kifupi iwezekanavyo.
“Ni dhahiri kuwa nyie wabia wetu mtanufaika na gesi asilia hiyo
kutokana na uwekezaji wenu lakini kimsingi tunataka gesi hii iwanufaishe
watu wetu, iwatoe katika umaskini. Kama gesi hiyo inaweza kutuingizia
pato la dola za Marekani bilioni moja kwa mwaka, ni dhahiri tunaweza
kuibadilisha nchi hii ikawa mbingu,” alisema.
Rais Kikwete aliongeza kuwa jukumu kubwa la gesi asilia nyingi
iliyogunduliwa na inayoendelea kugunduliwa maeneo mbalimbali nchini ni
kuwatoa Watanzania katika umaskini.
Naye Finlayson alisema maendeleo ya maandalizi ya uchimbaji wa gesi
asilia hiyo, itakuwa ni pamoja na kutoa nafasi za masomo kwa vijana wa
Kitanzania kusomea utaalamu mbalimbali wa gesi hiyo asilia.
No comments:
Post a Comment