HATIMAYE mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara wamefikia muafaka na
mshambuliaji wao wa kimataifa, Mganda Hamis Kiiza na tayari mmoja ya
wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo amekwenda nchini Uganda
kumsainisha mkataba mpya hivyo kuendelea kukipiga Jangwani.
Awali, Kiiza aligoma kuongeza mkataba mpya kwa madai ya kutokubaliana
na dau la dola 35,000 ili aongeze mkataba mwingine wa kuitumikia klabu
hiyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya
Mashindano ya Yanga, Abdallah Bin Kleb, alisema baada ya mazungumzo ya
muda mrefu hatimaye Kiiza amekubali kuongeza mkataba mpya, hivyo nyota
huyo ni mali yao.
Alisema nyota huyo atasaini mkataba wa miaka miwili akiwa kwao Uganda
kabla ya kuja nchini baadaye ili kuendelea kuitumikia klabu yake hiyo.
Hata hivyo, Bin Kleb hakuwa tayari kutaja dau walilomuongezea nyota
huyo, ingawa taarifa za uhakika kutoka Yanga zinasema nyota huyo
aliyetua Jangwani misimu miwili iliyopita akitokea URA, ameongezewa
dola 5,000 zaidi, hivyo thamani yake kufikia dola 40,000.
Aidha, imeelezwa kuwa, Kiiza atalipwa fedha hizo kwa awamu mbili
ambapo atalipwa kwanza dola 20,000 na baadaye kumaliziwa dola 20,000.
Hivi karibuni, uongozi wa Yanga ulikuwa ukihaha kumsainisha mkataba
mpya nyota huyo ambaye pia anakipiga timu ya taifa ya Uganda, ‘Uganda
Cranes,’ lakini nyota huyo aliendelea kuweka ngumu kusaini kwa dola
35,000 za Marekani zilizokuwa zimewekwa mezani.
Kiiza, mtoto wa askari wa zamani wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), aliyepigana vita ya Idd Amini mwaka 1978/9 na kulowea huko akioa
raia wa huko, ni miongoni mwa nyota mahiri katika kikosi cha Yanga,
akichangia kwa kiasi kikubwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame Julai 28,
mwaka 2012 na ubingwa wa Ligi Kuu Mei 18, 2013.
No comments:
Post a Comment