TIMU ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, inaweza kufananishwa na sikio
la kufa ambalo kamwe huwa halisikii dawa, licha ya juhudi kubwa za
kusaka tiba.
Ndivyo ilivyo kwa timu hiyo ambayo baada ya Juni 8 kupoteza nafasi ya
kucheza fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil, jana imeshindwa tena
kupata tiketi ya fainali za Afrika kwa nyota wa Ligi za Ndani-CHAN.
Kipigo cha siku hiyo cha mabao 4-2 kutoka kwa Ivory Coast kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kikafuta hesabu za Brazil, hivyo
turufu pekee ilikuwa ni fainali za CHAN nchini Afrika Kusini, pia za
mwakani.
Katika mechi ya jana iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Mandela,
mjini Namboole, nje kidogo ya Kampala, Stars wakiwa nyuma kwa bao 1-0
walilofungwa Julai 13, jijini Dar es Salaam, walifungwa tena 3-1.
Kwa idadi ya mabao 4-1, si tu imeitupa Stars nje ya vita hiyo ya
kwenda Brazil na kuipa Uganda tiketi ya Afrika Kusini, pia imetoa jawabu
kwamba kazi kubwa inahitajika ili kuwa na timu bora.
Stars iliyocheza fainali za kwanza nchini Ivory Coast mwaka 2009 chini
ya Mbrazil Marcio Maximo, ilimaliza kipindi cha kwanza kwa sare ya bao
1-1.
Wenyeji walianza kufunga bao dakika ya saba katika mechi
iliyochezeshwa na Kanoso Abdoul Ohabee kutoka Madagascar, likifungwa na
Frank Kalanda, akimalizia mpira uliopigwa ndani
ya eneo la hatari la Stars.
Bao hilo liliwafanya Stars watulie zaidi na kufanikiwa kusawazisha
dakika ya 18, mfungaji akiwa Amri Kiemba kutokana na pasi nzuri ya
Mrisho Ngasa kwenye kona ya eneo la mita 18.
Dakika ya 32 nusura Stars ipate bao, lakini mkwaju maridadi wa Ngasa
ambao tayari ulikuwa umempira kipa Hamza Muwonge, uligonga mwamba kabla
ya kuokolewa na mabeki.
Bao la pili la wenyeji katika mechi hiyo lilifungwa dakika ya 48 na
Brian Majwega, kabla ya Kalanda kuongeza la tatu dakika ya 63, kutokana
na makosa ya Salum Abubakar kupokwa mpira akiwa kwenye nafasi nzuri ya
kutoa pasi kwa mwenzake.
Kocha Kim Poulsen alifanya mabadiliko dakika ya 43, akimwingiza Simon
Msuva badala ya Frank Domayo aliyeumia na dakika ya 78 akawaingiza kwa
mpigo Haruna Chanongo na Vincent Barnabas na kuwatoa David Luhende na
John Bocco.
Hata hivyo mabadiliko hayo hayakubadili matokeo ya mchezo ambapo hadi
mwisho wenyeji Uganda waliibuka na ushindi wa mabao 3-1, hivyo
kujitwalia tiketi ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-1.
Kikosi cha Stars kilipangwa hivi: Juma Kaseja, Erasto Nyoni, David
Luhende/Vincent Barnabas, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Athuman Idd,
Frank Domayo/Simon Msuva, Salum Abubakar, John Bocco/Haruni Chanongo,
Amri Kiemba na Mrisho Ngasa.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itarejea nyumbani leo saa 4 usiku kwa ndege ya Precision Air.
No comments:
Post a Comment