MBUNGE wa Viti Maalumu (CHADEMA), Suzan Lyimo, amesema suala
la ukaguzi wa elimu shuleni limekuwa tatizo kutokana na wakaguzi
kutengewa bajeti ndogo.
Hayo aliyasema jana jijini Dar es Salaam, katika kikao maalumu cha
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni,
kilichojadili taarifa ya utendaji na uwajibikaji wa halmashauri hiyo kwa
mwaka 2012 na 2013.
Lyimo alisema wakaguzi wanatengewa bajeti ya sh mil. 4 kwa mwezi kiasi
ambacho ni kidogo kwa kuwa wanahitaji bajeti ya sh mil. 100.
“Kipindi cha nyuma kitengo hicho kilikuwa kinafanya kazi kwa ufanisi
lakini sasa hivi bajeti ni ndogo huku wakikosa magari, hatua
inayochangia wakaguzi hao kukaa ofisini bila kwenda kukagua shule,”
alisema Lyimo.
Alisema serikali isitegemee miujiza katika elimu kutokana na kushindwa kuwathamini wakaguzi wa elimu nchini.
Naye, Diwani wa Kata ya Sinza, Renatus Pamba (CHADEMA), aliitupia
lawama manispaa hiyo kwa kushindwa kuwashirikisha viongozi wa kata hiyo
katika utoaji wa leseni za uanzishaji na uendeshwaji wa baa.
Alikwenda mbali na kuitaja miongoni mwa baa ambazo ni kero kwa
wananchi na hazijafuata taratibu kwamba ni ‘Shikamoo pesa’ iliyopo
maeneo ya kata hiyo, ambapo kontena limewekwa barabarani na ni eneo la
wazi.
Alisema anashangazwa na viongozi wa manispaa hiyo kushindwa kuichukulia hatua za kisheria.
No comments:
Post a Comment