WAZIRI wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amewasihi Watanzania
wazuie katiba mpya isitoe rais dikteta na mwenye kutumia madaraka vibaya
kwa kuinufaisha familia yake au jamaa walio karibu naye.
Sitta amesema analiona taifa linaelekea kwenye hatari kubwa, kwamba
baadhi ya viongozi wanahangaika kuingiza mambo binafsi yenye maslahi
ndani ya rasimu ya katiba mpya badala ya kuangalia utaifa.
“Hawa wanaoingiza mambo yao binafsi si watu wazuri kwa taifa letu,
tukiwaacha waendelee na mchezo wao katiba mpya itakuwa chungu sana
kwetu,” alisema.
Sitta alisema Watanzania wanatakiwa kutengeneza katiba nzuri
itakayomzuia rais atakayechaguliwa kuwa mroho na kutumia madaraka yake
kuinufaisha familia yake au jamaa walio karibu naye.
Kiongozi huyo alitoa onyo hilo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa
akifungua mkutano wa Baraza la Taifa la Vijana la Rasimu ya Katiba mpya
unaotarajia kumalizika kesho.
Sitta alisema misingi ya utawala bora ndiyo silaha kubwa ya
kuhakikisha viongozi wanaochaguliwa hawafanyi kazi kwa udikteta au
masilahi binafsi.
“Nawasihi ndugu zangu tusikubali katiba mpya ijayo ikachezewa na
wajanja wachache maana tukifanya hivyo kuna hatari tukatengeneza rais na
serikali ya kidikteta” alisema.
Alisema kwa muda mrefu Tanzania imekuwa na historia ya kufuata misingi
ya utawala bora hivyo ni vizuri jambo hilo likaendelezwa.
Sitta alibainisha kuwa katiba ni muhimu kwa mustakabali wa Tanzania na
lazima wananchi wajenge utamaduni kuiheshimu na kuilinda huku
wakiwaepuka watu wanaotaka kuwania madaraka kwa masilahi binafsi.
“Tunahitaji kiongozi mwenye kujali masilahi ya Watanzania, hatuhitaji
yule mwenye kujali tumbo lake au la familia yake, haya yote yatafanikiwa
kama tutaweka vipengele kwenye katiba yetu itakayowabana watu wa aina
hiyo,” alisema.
Muundo wa Muungano
Waziri Sitta alisema rasimu ya katiba mpya ilenge kupunguza gharama
za uendeshaji wake kwa sababu Watanzania ni masikini na wanahitaji
maendeleo.
Alibainisha kuwa hakubaliani na mapendekezo ya rasimu ya katiba mpya
iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya uwepo wa mawaziri 15
kwenye Serikali ya Muungano ilhali mambo ya Muungano yapo saba.
Aliongeza kuwa wabunge 150 na mawaziri 15 wa Serikali ya Muungano ni
kutapanya fedha za walipakodi wanadidimia kwenye lindi la umasikini.
“Wananchi wanahitaji maendeleo, tujikite kupunguza matumizi na mbwembwe mbwembwe zisizo na tija kwa taifa,” alisema.
Alisema nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikisuasua kupiga hatua kwenye
maendeleo kwa kuwa fedha nyingi zinatumika kwenye uendeshaji wa serikali
badala ya kupelekwa katika sekta zenye kuwainua kiuchumi wananchi.
Apinga marais watatu
Sitta alipendekeza kuwa kama muundo wa serikali tatu unaopigiwa debe
na baadhi ya watu utafanikiwa ni vema vyeo vya marais wawili wa Zanzibar
na Tanganyika vikafutwa ili kuiepusha nchi kuwa na marais watatu.
Alisema nchi mbalimbali zitaicheka Tanzania kama itakuwa na marais watatu ambao wote inaweza ikatokea wakakutana nje ya nchi.
“Tutakuwa watu wa ajabu sana huko kwa wenzetu, yaani sisi masikini
halafu tuna marais watatu? Hizi gharama tunazotaka kumtwishwa mwananchi
za nini?” alihoji.
Alisema kama kutakuwa na serikali tatu ni vema kukawepo na rais mmoja
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wengine wakapewa majina mengine
kama Makamu wa Rais au Waziri Mkuu.
Sitta aliongeza kuwa hapingi muundo wa serikali tatu, bali hakubaliani na hoja ya uwepo wa marais watatu.
Aliongeza kuwa hoja ya kutaka marais hao watatu inashabikiwa na wenye
uroho wa madaraka, wanaodhani inaweza kuwa njia rahisi kwao kufikia
malengo yao ya kisiasa.
“Kuna watu wana kiu kubwa ya kuitwa mheshimiwa rais, ndiyo maana
wanapigia debe uwepo wa marais watatu, nawaona ni wabinafsi tu hawana
jambo jingine,” alisema.
No comments:
Post a Comment