Habari na Tanzania Daima.
JESHI la Polisi Mkoa wa Kinondoni linatuhumiwa kumuua Selemani
Mwinyi Msanga, mkazi wa Kurasini, jijini Dar es Salaam akiwa katika
Kituo cha Polisi Oysterbay.
Msanga anadaiwa kuuawa kati ya Julai 18-20 baada ya kukamatwa na
askari wa jeshi hilo na kisha mwili wake kwenda kuhifadhiwa katika
Hospitali ya Mwananyamala.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Mwananyamala
jana, ndugu wa Msanga, Joachim Mgende na Nasoro Msanga walisema Julai
18 walipata taarifa ya ndugu yao alikamatwa na kuambiwa wamfuatiliae
katika Kituo cha Polisi Oysterbay.
Alisema siku ya kukamatwa kwa Msanga askari waliovaa kiraia walifika
nyumbani kwa marehemu Kurasini na kufanya upekuzi huku wakiwa wanampiga
na fimbo ya ufagio wakiochukua uani mwa nyumba hiyo.
Aliongeza wakati wa tukio hilo mtoto wa kufikia wa Msanga
alishuhudia hali hiyo na kumpigia simu mama yake aliyekuwa eneo la
Kigogo katika msiba na kumueleza kuwa baba yake amepigwa na kuchukuliwa
katika gari na watu waliojitambulisha kuwa ni askari wanaotoka
Oysterbay.
“Baada ya taarifa hizo wanandugu tulifuatilia huko Oysterbay
tukaambiwa yupo Sitakishari nako tukaenda wakatuambia hajafikishwa,
ilikuwa ni kuzungushwa tu mpaka tulipokuja kupata taarifa kuwa yupo
chumba cha maiti Mwananyamala.
Alisema Julai 21 ikiwa ni siku ya nne kufuatilia hatima ya ndugu yao,
dada wa marehemu alifika katika Kituo cha Oysterbay na kuonana na
baadhi ya askari akiwamo mkuu wa kituo hicho, ambapo walimueleza kuwa
hawana taarifa ya mtu huyo na kuwataka warejee kesho yake (Jumatatu) kwa
taarifa zaidi.
Aliongeza kuwa baada ya taarifa hizo ndugu hao wakiwa wanajiandaa
kuondoka kituoni hapo walifuatwa na mmoja wa askari wa kike na kuwaeleza
kuwa ndugu yao amefariki dunia na kwamba mwili umehifadhiwa Hospitali
ya Mwananyamala.
“Tulikaa kikao na kwenda Mwananyamala pale tukaomba kuuona mwili wa
ndugu yetu huku tukisema polisi wametuambia umehifadhiwa pale. Kwa kweli
hatukuweza kuutambua kwa urahisi, kwani ulikuwa umevimba na kupoteza
uhalisia wake, kilichotusaidia ni kwamba baba mdogo alikuwa na alama
usoni (sunzua) ndiyo tukamtambua,” alisema Nasoro.
Nasoro aliongeza kuwa kinachowasikitisha ni kuona Jeshi la Polisi
linalotegemewa kuwa chanzo cha watu kufuata sheria likiwa mstari wa
mbele kuvunja sheria.
Alisema hata kama ndugu yao alikuwa na tuhuma ambayo hawaifahamu,
ingekuwa vema kama angefikishwa katika vyombo vinavyotafsiri sheria ili
vimhukumu badala ya kukatisha uhai wake kwa njia ya kipigo.
Tanzania Daima ilifanikiwa kuona taarifa zilizotumika kwa ajili ya
kuuhifadhi mwili wa Msanga katika chumba cha maiti ambazo zilikuwa
zinaonyesha marehemu akiwa hajulikani jina na kwamba mwili wake
uliokotwa katika eneo la Msasani.
Aidha, ripoti ya daktari iliyotolewa kwa ndugu wa marehemu ilionyesha kuwa sababu za kifo hicho hazijulikani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alipoulizwa juu
ya kumshikilia Msanga na hatimaye kupoteza maisha akiwa kituoni alisema
hana taarifa hizo na kwamba atazifanyia kazi.
Alipoulizwa kama anajua juu ya mtu aliyeokotwa katika eneo la Msasani
akiwa amefariki dunia, pia kamanda huyo alisema atafanyia kazi na kutoa
taarifa sahihi.
“Mimi siyo kamanda mbabaishaji na sifanyi kazi kwa kuendeshwa na
mwandishi, nimekupokeeni nitafanyia kazi hayo mliyoniuliza na nitatoa
majibu kwa ajili ya faida ya taifa,” alisema Wambura.
Wakati huo huo, wahudumu wa chumba cha maiti katika Hospitali ya
Mwananyamala jana waliwakatalia askari wa Jeshi la Polisi kuingiza maiti
katika chumba cha maiti kwenye hospitali hiyo kwa madai kuwa wamechoka
kupokea miili ya watu waliokufa kutoka katika Kituo cha Oysterbay.
Tukio hilo lilitokea wakati waandishi wa habari wakipata maelezo juu
ya madai ya kuuawa kwa Msanga, ambapo katikati ya maelezo hayo polisi
waliwasili na mwili wa mtu na kutaka kuuhifadhi kabla ya kukataliwa na
kuamua kuondoka nao.
Mmoja wa askari aliyeusindikiza mwili huo alisikika akiwaambia wenzie
waondoke kwa kuwa miili inayotoka Oystebay Polisi haiwezi kupokewa
katika hospitali hiyo.
Katibu wa hospitali hiyo aliyekataa kutaja jina lake, alipoulizwa
sababu ya kukataa miili inayotoka Kituo cha Polisi Oysterbay alisema
suala hilo hana taarifa nalo na kuomba apewe muda wa dakika tano
afuatilie.
Baada ya dakika tano katibu huyo alirudi na kuwaeleza waandishi kuwa
taarifa rasmi zitatolewa leo huku akisisitiza kuwa taratibu za hospitali
lazima zizingatiwe katika kuhifadhi miili inayotoka nje.
No comments:
Post a Comment