

Njiwa akiwa amedhoofu kwa Baridi akiwa katika choo cha wanaume
Hii ni sehemu alipokutwa Njiwa huyo
Majengo
Baadhi ya wafanyakazi wakielekea eneo la tukio
Afisa Mwajiri (Mwenye shati ya bluu) Na baadhi ya wafanyakazi wakishuhudia tukio
Mashuhuda wakitoka eneo la tukio
Stesheni ya TAZARA kituo cha Mbeya
--------------
WAFANYAKAZI
wa Mamlaka ya Reli, kati ya Tanzania na Zambia(TAZARA) jana walijikuta
katika wakati mgumu na baadhi yao kulazimika kuzikimbia ofisi zao, baada
ya ndege aina ya njiwa kukutuwa katika moja ya choo cha ofisi hiyo
akiwa amefungwa hirizi shingoni, huku akiwa na barua yenye ujumbe wa
onyo kali.
Tukio hilo la aina yake, lilitokea mapema saa mbili asubuhi katika
ofisi za mamlaka hiyo zilizopo eneo la Iyunga Mkoani hapa, hali ambayo
mbali na baadhi ya wafanyakazi wake kuzikimbia ofisi, ilisababisha
kuibuka kwa mjadala mkubwa dhidi ya tukio hilo.
Mtandao huu ulifanikiwa kushudia njiwa huyo mweusi akiwa nyuma ya choo
cha kiume katika eneo hilo la ofisi ya mwajiri, huku akiwa amefungwa
hirizi shingoni iliyozungushiwa shanga mchanganyiko wa rangi tatu,
ambazo ni Nyekundu, Njano na Nyeupe.
Mbali ya kuwa na hirizi hiyo, pia njiwa huyo alikuwa amebeba barua
inayodaiwa kuwa ni ya mmoja wa wafanyakazi wa Mamlaka hiyo (jina
limehifadhiwa kwa sababu maalumu) ambaye anadaiwa hivi karibuni
kufukuzwa kazi kwa makosa ya ubadhirifu.
Barua hiyo ilikuwa na maandishi mekundu yenye ujumbe ulioandikwa kwa
lugha mbili za Kiswahili na kiarabu, ambapo katika maandishi ya
Kiswahili yalisomeka :
"Naomba majibu haraka kama mtarudisha binti huyu kazini”. ilisema sehemu
ya ujumbe huo, huku ikiwa na orodha ya majina matatu ya viongozi wa
shirika hilo.
Mbali na ujumbe huo ukiwa umeandikwa kwa maandishi ya mkono
yaliyokolezwa kwa wino mwekundu upande wa nyuma, lakini upande wa mbele
kulikuwa na maandishi yakiwa ni barua ya kutaarifiwa kufukuzwa kazi kwa
mfanyakazi huyo.
Akizungumzia tukio hilo, Mwajiri wa mamlaka hiyo kanda ya Mbeya,
aliyejitambulisha kwa jina la Mchaba Mgweno, alikiri kutokea kwa tukio
hilo na kwamba waliobaini ni wahudumu wa usafi.
Aliongeza kuwa baada ya kupokea taarifa hiyo aliwaarifu na wafanyakazi
wenzake ambao walikusanyika na kumshuhudia Njiwa huyo mweusi akiwa
amedhoofika huku akiwa na barua hiyo yenye vitisho.
Alisema baada ya kushuhudia hali hiyo waliamua kutoa taarifa kituo cha
polisi kilichopo ndani ya shirika hilo, ambapo waliichukua barua hiyo na
baadhi ya wafanyakazi hao wakienda kutoa maelezo kituoni hapo.
“Kwa kweli hali hii si ya kawaida, ila kwa sasa siwezizungumzia chochote
kwa kuwa hata mimi tukio hili limeniweka katika wakati mgumu na
nimeshindwa kuendelea na majukumu yangu ” alisema Mgweno.
Hata hivyo kuliibuka malumbano makali kati ya wafanyakazi wa shirika
hilo walioshuhudia tukio hilo, ambapo baadhi yao wakidai kuwa tukio hilo
ni la kutengenezwa kwa lengo la kuchafuana.
“Hebu angalia hiyo barua yenyewe mbona ni kivuli (Photocopy), kama
ingekuwa ni ya ….wanamtaja mfanyakazi aliyefukuzwa jina limehifadhiwa
ingekuwa ni nakala halisi….haiwezekani mambo haya ni kutaka kuchafuana
tu” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Lakini baadhi yao waliamini kweli kuwa barua hiyo ilitumwa ili itoe vitisho kwa viongozi wa shirika hilo.
Baadhi ya askari polisi wa kituo cha Tazara walikiri kutokea kwa tukio
hilo na kwamba wanaendelea na uchunguzi ili kubaini ukweli wake.
“Ndugu zangu nyie mnajua taratibu za utoaji wa taarifa kwa jeshi hili,
maana wapo wahusika, lakini kwa kifupi sisi tulipokea taarifa na
tunaendelea kuzifanyia kazi” alisema mmoja wa askari hao.
Hata hivyo, hadi tunapoondoka eneo la tukio majira ya saa sita mchana Njiwa huyo alikuwa bado yupo eneo la tukio.
No comments:
Post a Comment