Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2013/2014 inaanza
kutimua vumbi kesho (Agosti 24 mwaka huu) katika viwanja saba tofauti
huku mabingwa watetezi Yanga wakianza kutetea ubingwa wao kwa
kuikaribisha Ashanti United kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro utakuwa mwenyeji wa
mechi kati ya Azam ya Dar es Salaam na wenyeji Mtibwa Sugar. Oljoro JKT
itaikaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta
Amri Abeid jijini Arusha.
Mgambo Shooting itaoneshana kazi na JKT Ruvu ambayo hivi sasa iko
chini ya Kocha Mbwana Makata. Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Mkwakwani,
Tanga wakati Rhino Rangers itakwaruzana na Simba katika Uwanja wa Ali
Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Mbeya City iliyopanda VPL msimu huu itapimana ubavu na Kagera Sugar
kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya huku Ruvu Shooting
ikiialika Mabatini, Mlandizi timu ya Tanzania Prisons kutoka Mbeya.
Mzunguko wa pili wa ligi hiyo utachezwa Agosti 28 mwaka huu. Baada ya
hapo ligi itasimama kupitisha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya
Gambia na Tanzania (Taifa Stars) itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu
jijini Banjul. VPL itaingia mzunguko wa tatu Septemba 14 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment