LONDON, ENGLAND
HATIMAYE Ligi ya Mabingwa Ulaya inarejea tena leo
Jumanne na kesho Jumatano katika viwanja mbalimbali barani Ulaya kwa
ajili ya mchakato wa kuivua taji Bayern Munich ambao ni mabingwa
watetezi.
Jijini Manchester, Manchester United itawakaribisha Bayer Leverkusen inayofundishwa na staa wa zamani wa Liverpool, Sami Hayypia, wakati katika kundi hilohilo la A, Real Sociedad ya Hispania itaikaribisha Shakhtar Donetsk ya Ukraine.
Katika Kundi B, Gareth Bale na Cristiano Ronaldo wataiongoza Real Madrid ugenini nchini Uturuki kukipiga na Galatasaray ambayo inaongozwa na mkongwe Didier Drogba. Na katika pambano jingine la kundi hilo, FC Copenhagen ya Denmark itaikaribisha Juventus ambayo kwa sasa mashambulizi yake yanaongozwa na Carlos Tevez.
Katika Kundi C, PSG iliyojaza mastaa kama Edinson Cavani na Zlatan Ibrahimovich itakuwa ugenini kupambana na Olimpiakos ya Ugiriki, wakati Benifica itakuwa nyumbani Ureno kukipiga na Anderlecht ya Ubelgiji.
Kocha Pep Guardiola ataanza kazi ya kutetea taji la Bayern Munich katika Kundi D wakati atakapokuwa nyumbani kuwaongoza wababe hao dhidi ya CSKA Moscow ya Urusi. Katika kundi hilo, Manuel Pellegrini ataiongoza Manchester City ugenini katika pambano dhidi ya Plazen ya Czech.
Jumatano
Katika Kundi E, Samuel Eto’o atarudi katika mechi
za Ligi ya Mabingwa kwa kuiongoza Chelsea katika pambano la nyumbani
dhidi ya FC Basel. Pambano jingine la kundi hilo, Schalke 04 ya
Ujerumani itaikaribisha Steaua Bucharest ya Romania.
Jijini Marseille, Mesut Ozil ataiongoza Arsenal
katika pambano lake la kwanza la Ligi ya Mabingwa dhidi ya Marseille
huku wababe hao wa London wakiwakosa, Santi Cazorla, Lukas Podolski na
Mikel Arteta.
Jijini Naples, Napoli watakuwa nyumbani kuwakaribisha Borussia Dortmund ya Ujerumani ambao msimu uliopita walifika fainali.
Katika Kundi G, Porto watakuwa ugenini
wakikaribishwa na Austria Wien, wakati Atletico Madrid watakuwa nyumbani
Hispania kukipiga na Zenit Petersburg ambayo inaongozwa na staa wa
zamani wa Arsenal, Andrey Arshavin.
Katika Kundi H, AC Milan ambayo imemrudisha mkali
wake wa zamani, Ricardo Kaka kutoka Real Madrid itakuwa nyumbani San
Siro kukipiga na Celtic ya Uskochi, wakati Lionel Messi na Neymar
watakuwa wakiongoza safu ya mashambulizi ya Barcelona dhidi ya Ajax
Amsterdam.
No comments:
Post a Comment