KOCHA wa Yanga, Ernie Brandts amelalamikia hali ya hewa ya Mbeya
kuwa ni nzito na inawafanya wachezaji wake wabanwe na pumzi wanapokuwa
uwanjani kwa kuwa ni tofauti na Dar es Salaam.
Sambamba na hilo bosi huyo amebadilisha programu ya mazoezi ili kwenda sambamba na hali ya Uwanja wa Sokoine ambao ni chakavu.
Brandts ameshusha pumzi baada ya kikosi chake kuimarika kwa ujio wa Mnyarwanda Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ aliyekuwa kwao Rwanda na pia atakuwa huru kumtumia, Simon Msuva ambaye alikuwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu, ilikuwa ni njano mbili alizopata katika mechi dhidi ya Coastal Union.
Wachezaji wote hao hawakucheza mechi ya Mbeya City na mapengo yao yalikuwa wazi na wanatarajiwa kuwa wapishi wa mastraika Mrundi Didier Kavumbagu na Jerry Tegete.
“Hawana majeruhi ingawa uwanja na hali ya hewa ndiyo kikwazo kwao hata hivyo tatizo hilo litakuwa limepungua kwani ndani ya siku hizi sita tangu walipofika Mbeya Jumatano wameonyesha kuzoea,’’ alisema Brandts.
Kuanzia juzi Jumapili iliyopita Yanga waliutumia Uwanja wa Sokoine kujifua kabla ya mechi hiyo ya kesho Jumatano. Brandts alisema: “Tumejiandaa kwa nafasi yetu kwa kufanyia marekebisho mapungufu ya mechi iliyopita ingawa uwanja bado ni tatizo kwetu. Nimefarijika kwa sababu nitakuwa na Niyonzima na Msuva aliyekuwa anatumikia kadi nyekundu.”
Katika hatua nyingine Brandts pia ameomba ulinzi mkali kwenye mechi hiyo: “Matatizo ni yale yale uwanja pamoja na hali ya vurugu, hivi vinachangia timu yangu kutocheza vizuri kwa sababu wanakuwa na hofu.”
Kocha wa Prisons, Jumanne Chale ambaye aliwasili Mbeya na kikosi chao jana Jumatatu mchana akitokea Tanga kucheza na Coastal Union waliyotoka nayo suluhu alisema uchovu ndiyo utata kwao lakini wamejidhatiti.
Brandts aliwataka wachezaji wake wacheze pasi za kugusa mara moja na si kuuchezea mpira,
kulingana na mazingira ya uwanja huo kuwasumbua. Pia anataka spidi, ushapu wa kutozubaa na mpira.
Kulingana na mazoezi na fomesheni ya Brandts ya 4-3-3 Ally Mustapha ‘Barthez’ atacheza kipa, Mnyarwanda Mbuyu Twite beki ya kulia na kushoto atakuwa David Luhende. Kelvin Yondani na Nadir Cannavaro watacheza beki ya kati.
Viungo watatu wa kati ni Athuman Idd ‘Chuji’, Niyonzima na Frank Domayo na washambuliaji watatu wa mwisho atakuwa ni Msuva, Kavumbagu na Tegete.
No comments:
Post a Comment