Habari na Tanzania Daima JUMAPILI.
WAKATI Rais Jakaya Kikwete akisubiriwa asaini Muswada wa
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013 ili iwe
sheria, viongozi wa upinzani nchini wameamua kuanza mchakato wa kumng’oa
kiongozi huyo, Tanzania Daima Jumapili limedokezwa.
Wenyeviti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman
Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi), leo
wanatarajia kukutana na wahariri na waandishi wa habari kueleza
mikakati na mbinu watakazozitumia kunusuru taifa lisiingie kwenye
utungaji wa Katiba mpya itakayobeba masilahi ya chama tawala.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa mikutano ya hadhara,
maandamano na elimu kwa umma juu ya athari ya muswada huo ni miongoni
mwa mbinu zitakazotumiwa kuhakikisha Rais Kikwete hasaini muswada huo au
serikali inapeleka tena mabadiliko ya sheria hiyo katika Bunge lijalo
iwapo rais atasaini.
Wapinzani wanadai kuwa serikali iliubadili kwa nguvu muswada huo kwa
kuondoa maoni muhimu ya wadau, pia walilalamikia kitendo cha wajumbe wa
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge kutokwenda Zanzibar
kuchukua maoni ya upande huo wa muungano.
Wakati wapinzani wakijipanga kuweka wazi mikakati ya kumshinikiza Rais
Kikwete asisaini muswada huo, wadau mbalimbali wamemtaka kiongozi huyo
atumie busara ili taifa lipate katiba itakayokuwa na manufaa kwa taifa
kuliko inavyoonekana itikadi za vyama kugubika mchakato huo.
Wiki iliyopita akiwa Dodoma, Mbowe alikionya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), kuwa wasitarajie kuwa kupitishwa kwa marekebisho ya muswada huo
ndiyo Katiba mpya, bali kura ya maoni ndiyo itakayoamua jambo hilo.
Tanzania Daima Jumapili imedokezwa kuwa wapinzani wamejipanga
kuhakikisha wananchi wanaitumia kura ya maoni kupinga mpango wa Rais
Kikwete na serikali yake kupitisha Katiba mpya yenye mwelekeo wa
kukibeba chama tawala.
Hoja za wapingaji
Kamati Maalumu ya Katiba, nayo imepinga marekebisho ya muswada huo
ikiainisha eneo mojawapo lenye tatizo ni kuruhusu asilimia 72 ya wajumbe
wa Bunge Maalumu la Katiba kubeba wanasiasa.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Khoti Kamanga, alisema iwapo Katiba
mpya itaundwa bila upungufu unaoonekana sasa kupatiwa ufumbuzi
itazalisha migogoro zaidi, itakayosababisha nchi kuingia kwenye
machafuko.
Alikosoa Kifungu cha 8 na Kifungu kidogo cha 4 na 5 cha muswada huo
kwamba vina kasoro, kwa kuruhusu wabunge wa Bunge la Katiba kufanya
uamuzi kwa wingi wa kura badala ya kutumika utaratibu wa theluthi mbili
kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, naye anapinga muswada
huo kwa madai kuwa una upungufu mkubwa, ukiwamo wa Zanzibar
kutoshirikishwa, pia kumpa nafasi kubwa rais kuteua watu kutoka katika
asasi mbalimbali badala ya watu hao kuteuliwa moja kwa moja na asasi au
asasi husika.
Hofu ya yaliyotokea Kenya
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wamelidokeza Tanzania Daima
Jumapili kuwa Tanzania inafuata njia iliyopitwa na Kenya katika kupata
katiba mpya, ambayo ilipatikana baada ya kutokea machafuko mwaka 2007
mara baada ya kufanyika uchaguzi mkuu.
Mwaka 2005, wananchi wa Kenya wakiongozwa na wanasiasa maarufu, Raila
Odinga na Kalonzo Musyoka, waliibwaga serikali ya rais mstaafu wa nchi
hiyo, Mwai Kibaki, katika kura ya maoni ya kuamua kuikubali au kuikataa
rasimu ya katiba iliyokuwa imependekezwa na utawala wa rais Kibaki.
Ni kutokana na matokeo ya kura hiyo, uchaguzi mkuu wa 2007 ulizaa
machafuko na mauaji ya mamia ya Wakenya wasiokuwa na hatia, baada ya
kushindikana kupatikana kwa katiba mpya, hivyo utawala wa Kibaki kuamua
kuitisha uchaguzi mkuu kwa kutumia katiba na sheria za uchaguzi za
zamani zilizokuwa zikilalamikiwa kwa muda mrefu.
Wachambuzi wa siasa hapa nchini wanasema kuwa mwenendo wa hivi
karibuni wa mchakato wa kuandika Katiba mpya ya Tanzania unaonesha
ishara za wazi za kutokea yaliyotokea nchini Kenya. Kwamba, kushindwa
kufikia mwafaka baina ya wabunge wa Bunge la Tanzania lililomaliza vikao
vyake hivi karibuni mjini Dodoma, kuhusu muundo wa Bunge Maalumu la
Katiba ni uthibitisho wa wazi wa matatizo yanayoweza kutokea siku za
usoni.
Bunge Maalumu la Katiba ndilo litakaloandaa rasimu ya mwisho ya Katiba
mpya itakayopelekwa kwa wananchi mapema mwakani kwa ajili ya kura ya
uamuzi, hivyo muundo wake na kukubalika kwake ni jambo muhimu na
linalohitaji mwafaka wa kitaifa.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA ilipeleka
mapendekezo ya kutaka uwakilishi wa Bunge hilo upanuliwe kutoka wajumbe
600 wa sasa na kuwa wajumbe 789 ili kulifanya bunge hilo lisihodhiwe na
wanasiasa ambao zaidi ya asilimia 70 ni wanachama wa CCM.
Hata hivyo, pendekezo hilo lilishindwa baada ya wabunge wa CCM kutumia
wingi wao katika Bunge hilo kuyakwamisha mapendekezo ya upinzani na
badala yake kuamua kuendelea na muundo wa sasa unaoipa CCM haki ya
kisheria ya kulihodhi Bunge la Katiba.
Wachambuzi hao wanatabiri kuwa kama Rais Jakaya Kikwete atakubaliana
na msimamo wa wabunge wa chama chake, kwa kuitia saini sheria ya
marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba na hatimaye kuwa na Bunge
la Katiba na baadaye kura ya maoni, basi kuna uwezekano katiba hiyo mpya
ikakataliwa na wananchi katika kura ya maoni kama ilivyokuwa kwa Kenya
mwaka 2005.
Kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba ya 2011, kama wananchi
wataikataa katiba inayopendekezwa, basi katiba ya zamani itaendelea
kutumika katika shughuli zote za nchi, ikiwamo kuendesha Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2015, jambo ambalo linapingwa vikali na viongozi, wanachama,
wafuasi wa vyama vya upinzani na wanaharakati.
Ni kutokana na mazingira haya wachambuzi wa masuala ya siasa nchini
wanaamini na kutabiri kuzuka kwa ghasia, machafuko na umwagikaji wa damu
kama ilivyotokea Kenya mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM), Bashiru Alli, anasema: “Tunakabiliwa na hatari mbele
yetu, maana tunakwenda kwenye kura ya maoni kuhusu Katiba mpya tukiwa
tumemeguka vipande vipande. Tulipaswa kufika huko tukiwa wamoja kama
taifa, tulipaswa kuwa na mwafaka wa kitaifa katika suala hili la katiba
ya nchi badala ya kwenda kwa kuongozwa na itikadi zetu za kisiasa,”
alieleza Bashiru na kuongeza:
“Machafuko na mauaji yaliyotokea Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa 2007
yalitokana na makosa ya utawala wa rais mstaafu wa nchi hiyo, Mwai
Kibaki, ambaye aliamua kuwadharau na kuwapuuza wananchi katika mchakato
wa kuunda katiba ya nchi yao kama inavyofanyika sasa nchini mwetu, hili
ni jambo la hatari sana,” alionya Bashiru.
Bashiru anasema kuwa ili kuufanya mchakato wa sasa wa Katiba mpya kuwa
wa wananchi na kuepusha kuiingiza nchi kwenye machafuko na mauaji ya
wananchi wasio na hatia, mchakato wote unapaswa kurudiwa.
“Ili yasitufike yaliyotokea Kenya, tunapaswa kuanza upya mchakato wa
Katiba mpya, wananchi wapewe fursa ya kuumiliki mchakato mzima. Kwa
mfano, wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanapaswa kuchaguliwa na
wananchi, si kuteuliwa. CCM na wapinzani wanataka wajumbe wapatikane kwa
kuteuliwa, mimi nasema huo si utaratibu sahihi, dhana ya Bunge la
Katiba inataka wajumbe wake wapatikane kwa kuchaguliwa na wananchi, si
kuteuliwa,” anabainisha Bashiru.
Ulivyopitishwa
Mjadala wa muswada huo uliopitishwa Ijumaa iliyopita na wabunge wengi
wakiwa wa CCM, ulizua tafrani bungeni iliyosababisha Kiongozi wa
Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph
Mbilinyi (CHADEMA) kutolewa nje na askari. Katika tafrani hiyo, baadhi
ya wabunge wa upinzani walirushiana makonde na maofisa usalama, huku
wabunge wote wa upinzani, isipokuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine
Mrema, wakiususia.
No comments:
Post a Comment