KLABU ya Yanga imeamua kumlipia nyota wake Mrisho Ngassa kiasi
cha sh mil. 45 alizotakiwa kuirejeshea Simba na Kamati ya Sheria na
Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
kwa sharti la kukipiga Jangwani kati ya miaka mitano au minne.
Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa, imemtaka Ngasa
arejeshe kiasi hicho ndani ya kipindi cha adhabu ya kukosa mechi tano za
Ligi Kuu, kiasi cha sh mil. 30 alizopewa abaki hata baada ya kipindi
chake cha mkopo akitokea Azam na fidia ya asilimia 50 ya kiasi cha fedha
hizo.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo na kuthibitishwa na mmoja wa
viongozi wake, wameamua kufanya hivyo kulinda kiwango cha mchezaji huyo
ambaye kama watamwachia jambo hilo, kuna hatari ya kushindwa kucheza
tena, hivyo kuwa pigo kwa mchezaji na timu ya Yanga.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa jambo hilo wameshalijadili hata kwenye
baadhi ya vikao vya Kamati ya Utendaji hivi karibuni kwamba klabu
itabeba mzigo huo kwa sharti kuwa mchezaji huyo aliyewahi kucheza Kagera
Sugar, Azam na Simba, atacheza Yanga kwa miaka mitano au minne.
Habari zinasema kama jambo hilo litapata baraka kutoka kwa viongozi
wote, watalipa fedha hizo kuepuka kumpoteza Ngassa ambapo nyota huyo
atazirejesha kwa kutumikia Jangwani kwa miaka miwili au mitatu zaidi ya
mkataba wake wa miaka miwili uliomng’oa Simba.
“Bado hatujafikia muafaka ila suala hili tumelizungumza, tukikubaliana
tutamlipia kisha yeye atatumikia fedha hizo kwa miaka hiyo ambayo
tutasema sisi,” kilidokeza chanzo hicho na kuongeza kuwa ni jambo
litakalohitaji ridhaa ya mchezaji mwenyewe kwani atashirikishwa.
Tanzania Daima ilipomtafuta Ngasa kwa njia ya simu jana kupata maoni
yake, simu yake ya kiganjani iliita bila ya majibu huku Katibu Mkuu wa
Klabu hiyo, Lawrance Mwalusako, akisema hana taarifa ya jambo hilo zaidi
ya rufaa waliyowasilisha TFF kupinga adhabu hiyo.
CREDIT TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment