CHAMA cha Netiboli Tanzania (CHANETA), kimeandaa mashindano kwa
wanaume ili kupata timu zitakazoliwakilisha taifa katika mashindano ya
ndani na nje ya nchi.
Akizungumza hivi karibuni jiji hapa, Mwenyekiti wa
CHANETA, Anna Kibira, alisema chama chake kimechukua hatua hiyo baada ya
kubaini kukosekana kwa hamasa ya wanaume katika ushiriki wa netiboli,
licha ya kuwepo kwa wenye vipaji na uwezo.
Mwenyekiti huyo alisema, maandalizi juu ya mashindano hayo kwa wanaume
yameshaanza na yanatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa, kabla ya kufanyika kwa mashindano hayo kutakuwa na
mafunzo kwa wanaume wanaopenda kucheza tayari wameshaviandikia vyama vya
mikoa kwa ajili ya kutafuta wachezaji watakohudhuria mafunzo hayo.
Kibira alitoa wito kwa viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya wilaya,
mkoa hadi taifa wakiwemo wanasiasa hasa wabunge, kutoa msaada wa hali na
mali ili kupata timu kwa ajili ya mchezo huo ambao umeonekana kukosa
mashabiki licha ya kuwa ni ajira kwa vijana.
Katika hatua nyingine, Kibira alisema, Septemba 24 mwaka huu, timu ya
vijana chini ya miaka 18 kutoka Afrika Kusini, itaanza ziara hapa
nchini, ambapo itavaana na timu ya vijana wa Tanzania na timu nyingine
zitakazotajwa hapo baadaye.
No comments:
Post a Comment