JITIHADA za Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe,
kuimarisha mitambo ya ukaguzi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA) ili kuwanasa wabeba dawa za kulevya (unga),
zimeanza kufifishwa baada ya mtandao kubuni mbinu mpya.
Wakati hali ikiwa hivyo, meli ya mizigo yenye usajili wa Tanzania
imekamatwa nchini Italia ikiwa na tani 30 za mihadarati aina ya bangi
yenye thamani ya sh bilioni 123.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, wafanyabiashara hao wa dawa za kulevya
tayari wameanza kuupa kisogo uwanja wa JNIA na badala yake kuelekeza
mikakati hiyo katika uwanja wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
“Hatua ya Mwakyembe kufunga mtambo JNIA imewashtua watu wengi na hivi
sasa tayari kuna watu watatu ninaowafahamu wameshaweka kambi hapa Moshi
kwa ajili ya kusuka mipango ya kusafirisha dawa hizo kwa kutumia uwanja
wa KIA,” kilisema chanzo chetu.
Mmoja kati ya watu wanaotajwa kufanya biashara hiyo ni raia wa Kenya,
Hussein Mombasa, ambaye ameomba uraia wa Tanzania kisha kufanikiwa
kufunga ndoa na Halima Mosha.
Kwa kujibu wa chanzo hicho Halima ni ndugu wa karibu na mhasibu mkuu
hazina ndogo mkoa wa Iringa, Twaha Mtalika, ambaye ni kaka wa mama yake.
Mkenya huyo mbali na kufanikiwa kupata uraia wa Tanzania anadaiwa pia kushirikiana na mkewe huyo kufanya biashara hiyo haramu.
Mombasa anadaiwa kumeza dawa aina ya cocaine kisha kusafiri nazo
katika nchi mbalimbali na kwamba karibu safari zote alizokuwa akizifanya
alikuwa akipitia katika uwanja wa JNIA bila tatizo kutokana na kuwa na
mtandao uliokuwa ukimkingia kifua pale uwanjani.
“Huyu Mkenya ameshafunga ndoa na huyu mwanamke tangu Julai 5, mwaka
huu, na wanaishi katika nyumba ya mjomba wa mkewe iliyoko Ilala Mtaa wa
Kilwa.
“Shughuli nyingi za kuingiza hizo dawa huzifanyia hapo na mjomba mtu
ameamua kuwaachia nyumba hiyo kwa sababu yeye anafanya kazi mkoani,”
kilisisitiza chanzo hicho.
Nchi ambazo Mkenya huyo anatajwa kusafiri kwa ajili ya kupeleka mzigo
akitokea jijini Dar es Salaam ni Hispania ambako alikwenda akipitia
uwanja wa JNIA na kurejea Mei mwaka huu, wakati mwaka jana alipeleka
dawa hizo Afrika Kusini na kurejea Machi.
Inadaiwa kuwa pamoja na ndoa ya Halima kufungwa kihalali lakini bado
mwanamke huyo anang’ang’ania kuendelea kuwa sehemu ya umiliki wa nyumba
iliyoko Moshi, aliyochuma na Dominick Ngowi ambaye aliishi naye awali na
kupata watoto wawili: Oliver Dominick (19) na Frank (18).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Moshi, Stella Mugasha, alishatoa hukumu
Agosti 19, 2011 na kuamuru watoto hao watakapotimiza umri wa miaka 18
wamilikishwe nyumba hiyo baada ya baba yao kufungua kesi ya madai
(gazeti hili lina nakala zote zikiwemo za hukumu).
Hata hivyo, tayari mtoto mkubwa, Oliver ameshakabidhiwa umiliki huo
siku chache zilizopita kwa niaba ya mwenzake mbele ya Mwenyekiti wa
Serikali ya Mtaa wa Sabasaba Kata ya Soweto, Pamela Shuma na ofisa
mtendaji katia hiyo, Gudila Kimboka.
Wakati Mkenya huyo akidaiwa kusafirisha unga kwenda nje ya nchi,
Halima anatajwa kuzisafirisha kwa ustadi mkubwa kwa njia ya mabasi na
kuzipeleka mkoani Tanga eneo la barabara ya 11, Namanga na Arusha, na
kwamba ameshafanya hivyo mara nyingi.
“Wakati mwingine Ilala kukikosekana mzigo, huenda kuzichukua katika
eneo la Magomeni Mapipa ambako kuna jumba moja la kifahari wakati kwa
mkoani huficha mzigo wao Moshi nyumbani kwa mwanamke mmoja maarufu
ambaye pia ni ndugu wa karibu wa Mombasa,” kilieleza chanzo kingine cha
habari.
Habari zaidi zinadai kuwa Halima amekuwa mstari wa mbele kukisaidia
chama kimoja maarufu cha siasa nchini ambako ni mmoja wa viongozi wa
wanawake mkoani Kilimanjaro.
Tanzania Daima, ilipomtafuta mjomba wa mwanamke huyo Twaha Mtalika ili
kutaka kupata ukweli wa madai ya nyumba yake kutumiwa kufanyia biashara
hiyo haramu, aling’aka na kueleza kutojua masuala hayo.
Twaha ambaye anadaiwa kuwepo jijini Dar es Salaam kimasomo alijibu kwa
mkato: “Mwambie huyo kijana aliyekutuma uniulize hayo azungumze na
mwanamke wake na asiniingize mimi katika masuala yao.”
Naye Halima alipoulizwa kuhusu madai hayo, alijielekeza zaidi kwenye
madai ya kuwahusu watoto wasimilikishwe nyumba wakati mahakama
ilishaamuru hilo.
Huku akikanusha madai ya kughushi cheti cha kuzaliwa cha mtoto wake wa
pili Frank kwa lengo la kumpunguza umri ili kuharibu mchakato wa
umiliki huo kwa kushirikiana na mjomba wake, pia alisema tuhuma za
kusafirisha unga si za kweli.
Meli yabambwa Italia
Taarifa za kukamatwa kwa meli hiyo ya MV Gold Star, zilichapishwa hivi karibuni kwenye gazeti la Daily Mail la nchini Uingereza.
Meli hiyo ambayo imesajiliwa Tanzania kwa upande wa Zanzibar ilikamatwa baada ya vyombo vya usalama vya nchi hiyo kupata taarifa kuwako kwa meli hiyo iliyokuwa na shehena hiyo.
Baada ya taarifa hizo Kikosi cha Coastgurd cha Italia, kilifuatilia
meli hiyo kwa kutumia helikopta na hatimaye kufanikiwa kuinasa.
Meli hiyo inadaiwa kuwa wakati inakamatwa ilikuwa na watu tisa baadaye
walijaribu kujitosa baharini, miongoni mwao wakiwemo mabaharia wawili,
mmoja akiwa raia wa Misri na mwingine wa Syria.
Hata hivyo, watu saba waliobakia uraia wao ulikuwa haujafahamika.
Chanzo hicho kilieleza kuwa shehena hiyo ya bangi imepakuliwa pwani ya Uturuki karibu na Italia.
Alipotafutwa Mkuu wa Interpol, Gustavs Babile ili kutoa ufafanuzi,
alisema ni kweli meli hiyo iliyosajiliwa Zanzibar ilikamatwa ikiwa na
bendera ya Tanzania.
“Hata hivyo siwezi kuzungumzia mengi kama unavyojua leo ni Jumapili niko nje ya ofisi lakini hizo ndizo taarifa ambazo ziko kwenye nyaraka ambazo tunazo,” alisema.
Baadhi ya Watanzania katika siku za hivi karibuni walinaswa na
mihadarati kwenye nchi mbalimbali za Afrika Kusini, Hong Kong na China.
Via Tanzania Daima.
Via Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment