Kiongozi wa mashtaka katika
mahakama ya kimataifa ya jinai ICC, Fatou Bensouda, amepata pigo jengine
baada ya mashahidi wengine wanne kujiondoa katika kesi dhidi ya Naibu
Rais wa Kenya William Ruto na mshtakiwa mwenzake Joshua Arap Sang.
Hili limetokesa siku moja tu kabla ya Bensouda
kuanza kuwasilisha mashahidi mbele ya mahakama siku ya Jumanne kesi
dhidi ya Ruto itakapoanza tena.
Mashahidi hao wanajumuisha manusura
wa moto ulioteketeza kanisa la Kiambaa mkoa wa Rift Valley na
kusababisha vifo vya watu 35 wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu
nchini Kenya mwaka 2007-2008
Bwana Ruto anatuhumiwa kwa kuchochea ghasia ili
kujinufaisha kisiasa wakati Sang akidaiwa kumsaidia Ruto kuafikia
malengo yake kwa kutumia kituo cha Redio alichokuwa anafanyia kazi
wakati wa ghasia hizo.
Hii sio mara ya kwanza kwa mashahidi kujiondoa
katika kesi dhidi ya washukiwa hawa. Wiki mbili zilizopita mashahidi
wengine wawili walijitokeza nchini Kenya wakidai kuwa wanalazimishwa na
upande wa Mashtaka kutoa ushahidi wa uongo dhidi ya wawili hao.
Wadadisi wanasema kuwa kujiondoa kwa mashahidi
katika kesi hii bila shaka kutaathiri uwezo wa kiongozi wa Mashtaka
Fatou Bensouda lakini amewahi kusikika akisema kuwa kwa mashahidi
kujiondoa katika kesi yake dhidi ya Ruto na Sang sio hoja.
Kesi dhidi ya Ruto iliakhirishwa wiki jana baada
ya upande wa mashtaka kusema kuwa hawajakuwa tayari kuwasilisha
mashahidi wao na hivyo kupewa muda na mahakama hadi siku ya Jumanne wiki
hii. CHANZO NI BBC SWAHILI.
No comments:
Post a Comment