ILIPOISHIA SEHEMU YA 2 Na IRENE MWAMFUPE NDAUKA
Mbali na ‘toilet paper’ pia kuna kikopo chenye vijiti vyenye pamba
za masikio kilikuwa kwenye stuli jirani na kitanda, lakini kwa muda huo
kilikuwa kimeanguka chini halafu vijiti vimebaki kama vitatu tu kwa maana
kwamba, aliyeingia kuchukua ‘toilet paper’ ndiyo huyohuyo aliyechota vijiti vya
pamba.Nilianza kuhisi kuwa sikuwa kwenye nyumba salama, lakini kwa
uthibitisho upi?Moyoni nikasema nitajua tu, mimi ndiyo mimi.
***
Nilikaa ndani kwangu hadi usiku ulipoingia, nikasema nibadili nguo
kwa kuvaa bukta na singilendi halafu nitoke kwenda kula gengeni kwani siku hiyo
sikuwa najisikia kupika chochote. Ni mara nyingi nilipenda kula gengeni.
Nilitoka, nikasimama mlangoni ili nifunge mlango wa chumbani,
nilipoangalia chini, upande wa wenzangu nilikuta nje ya mlango wao pana vijiti
vya pamba za masikioni vikiwa vimetumika, nikiwa katika mshango, mbele nikaona
tishu ikiwa imefutiwa majimaji yenye rangi nyekundu kama damu.
Nilitembea kwa wasiwasi, nikatoka nje, sikufunga mlango kwa
funguo, lakini niliubamiza tu, funguo nilikuwa nazo, nikaenda gengeni kula.
Pale kwenye genge ambapo si mbali sana na nyumbani, alikuja yule
mama aliyeniuliza mimi ni mtu wa wapi, nilisalimia, lakini kabla hajaitikia
alishtuka kuniona.
“Upo kijana wangu?”
“Nipo mama, nimetoka kazini nimekuja kupata kidogo.”
“Pole sana, uoe sasa.”
“Huo ndiyo mpango wangu mama.”
“Ee, uoe halafu mimi nitakupa vyumba viwili pale kwangu,
nakuahidi.”
“Nashukuru sana mama. Naanza kujipanga.”
“Sawa, vipi wenzako lakini?”
Nilisita kumjibu, nikabaki namwangalia tu, naye alibaini kwamba
nimepata mshtuko na swali lake.
“Vipi wapangaji wenzako, naamini utakuwa hujaonana nao?”
“Ni kweli mama, tena hebu nakuomba kidogo,” nilisema nikienda
pembeni kidogo ili na yeye anifuate tukaongee.
“Niambie,” alianza kusema.
Nilimuuliza kama kuna anachokijua chochote kile kuhusu wale
wapangaji wenzangu. Alianza kwa kusema:
“Kusema ule ukweli sina kwa undani, ila napenda kukwambia kwamba,
unaishi na watu ambao unahitajika moyo wa ziada ili uweze kuendelea kuishi nao.
“Pale mbali na wewe, pameshakaa wapangaji wengine saba, tena wote
kama wewe, hawajaoa. Lakini kinachoshangaza ni kwamba, wanaondoka baada ya wiki
mbili, mmoja aliondoka baada ya siku tatu tu.”
“Kwa hiyo hakuna hata mmoja aliyewahi kukwambia ameona nini kule
ndani?”
“Hakuna.”
“Lo! Mimi mama mambo ninayoyaona yanatisha.”
“Kama mambo yapi, nisimulie kidogo.”
Nilipotaka kuanza kumsimulia huyu mwanamke, ghafla alitokea
msichana mmoja, mweupe, mrefu kiasi, amejazia sehemu mbalimbali za mwili,
akaniguna na kusema:
“Kama Humuli mambo vipi, za siku?”
Nilipata kigugumizi kikubwa kumjibu mambo poa kwani sikumjua na
sikuwa nakumbuka chochote kuhusu yeye, sura yake ilikataa kichwani mwangu.
“Wewe ni nani kwani?” nilimuuliza.
Akaachia tabasamu kwa mbali, uzuri wake ukaongezeka.
“Ha! Humuli, hunikumbuki mimi, kweli?”
“Sasa we binti, kama wewe ndiyo unamkumbuka si umkumbushe mlionana
wapi?” yule mwanamke alisema kwa sauti ya mshangao.
Lakini yule msichana mrembo alimwangalia yule mwanamke kwa macho
yaliyojaa hasira…
“Mama uhusiki.”
“Najua, lakini unapoteza muda kwa kuzungushazungusha wakati kumbe
wewe unamkumbuka, yeye umeshajua hakukumbuki na amekwambia tayari.”
Nilishangaa kumwona yule msichana akibetua kichwa kama aliyekuwa
akiweka vizuri nywele zake, ghafla yule mwanamke niliyekuwa naye akajishika
kichwa na kulalamika kinamuuma sana.
“Jamani kichwa! Kichwa jamani, daa!”
“Vipi mama, imekuwaje kwani?” nilimuuliza.
“Kichwa Humuli, kinavuta ghafla! Uwiii.”
Nilianza kuogopa, nilihisi naangukiwa na msala maana akifa pale na
watu waliona nikienda naye pembeni si nitahojiwa mimi?
“Kwani mama una kawaida ya kuumwa kichwa?” nilimuuliza
nikimsogelea ambapo yeye sasa alikuwa ameinama.
“Sina, ndiyo nashangaa hapa.”
Niliona hakuna dawa nyingine zaidi ya kumpeleka kwake ili
nikaungane na familia yake kumpeleka hospitali. Lakini kabla ya kufanya hivyo
niliinua macho ili nimwambie yule dada anisaidie na kama anataka kunikumbusha,
hayo yangefanyika baadaye.
Ile naanaza kusema anti huku nikiwa nimeinua macho, nilishangaa
kutomwona yule msichana pale.
“Khaa!” nilijikuta nikisema hivyo.
“Mama twende nyumbani ili tukupeleke hospitali na watoto wako.”
“Ha! Mbona kimeachia,” alisema akionekana kushangaa na kuniangalia,
alikuwa amepanua kunywa.
“Kweli?”
“Eee, niko mzima kabisa.”
“Au?” nilitaka kusema neno lakini zikulimaliza, nikahisi ulimi
unakuwa mzito si kwa kushikwa bali kwa matakwa yangu.
“Humuli.”
“Naam.”
“Ni kweli yule binti humjui?”
“Simjui mama.”
“Kuna mawili hapo, humjui au humkumbuki.”
“Vyote mama, simkumbuki na pia simjui.”
“Lakini wewe si alikutaja kwa jina?”
“Mwenyewe nilishangaa sana.”
“Basi Humuli nimeshaelewa, kwaheri, nimeelawa ni kwanini nimeugua
kichwa na yule ni nani, pole sana wewe kijana,” alisema yule mwanamke huku
akiondoka zake kuelekea kwake.
Nilimtazama, lakini
baadaye nilirudi kwenye kibanda cha chipsi.
“Mzee nakuona na miss jini,” muuza chipsi mmoja alisema.
“Yupi, yule mwanamke?”
“Hapana, yule msichana.”
“Mi simjui, kwani anaishi wapi? Maana kasema ananijua, ameniita na
jina.”
“Khaa! Kumbe wewe kama sisi. Huyu dada anaishi mitaa hiihii,
lakini hakuna hata mmoja anayejua nyumba anayoishi!
“Kuna jamaa mmoja anaitwa Maleke, Maleke aliwahi kumfuatilia kwa
nyuma lakini alishindwa kujua aliingia nyumba gani!”
“Mh! Au jini?” niliuliza kwa mshtuko mkubwa.
“Ndivyo watu wanavyosema, sasa alipokuja kusimama na wewe, tukawa
tunabishana, wengine wanasema ni miss jini, wengine siye, lakini alipokuwa
anaondoka tukagundua ni miss jini.”
Basi, tuliishia hapo, nikachukua chipsi zangu na kwenda nazo
nyumbani, niliamua kwenda kulia kule.
Nilifika, nikasukuma mlango mkubwa nikazama ndani kwangu. Lakini
wakati napita kwenye usawa wa chumba cha wale wenzangu nikasikia vicheko, tena
vicheko kwelikweli.
Sikuwajali, nikaingia sebuleni kwangu, nikafunga mlango kwa ndani,
nikaweka chipsi juu ya meza, nikaenda pembeni ya chumba ambako kuna ndoo ya
maji ili nichote ya kunawa.
Wakati naanza kula nilihisi na kugundua kitu. Niligundua
mabakimabaki ya chipsi na kuku juu ya meza yangu wakati ukweli ni kwamba, tangu
nimehamia pale sijawahi kula chipsi wala kuku.
“Humu ndani kuna mtu anaingia kufanya mambo yake, lini mimi
nimekula chipsi na kuku humu ndani?” nilijiuliza, nikasikia kicheko kutoka kwa
wenzangu.
“Haa! Haaa! Ha! Haaaa…aaaa.”
Niliinua macho kuangalia juu kwenye ‘silingbodi’ kama vile
niliyekuwa nimeona kitu, akiliza yangu ikawaza kitu cha dakika chache nyuma,
nacho ni hiki:
“Humuli.”
“Naam.”
“Ni kweli yule binti humjui?”
“Simjui mama.”
“Kuna mawili hapo, humjui au humkumbuki.”
“Vyote mama, simkumbuki na pia simjui.”
“Lakini wewe si alikutaja kwa jina?”
“Mwenyewe nilishangaa sana.”
“Basi Humuli nimeshaelewa, kwaheri, nimeelawa ni kwanini nimeugua
kichwa na yule ni nani, pole sana wewe kijana.”
Nilianza kuamini kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya yule
msichana na wale wapangaji wa pale ndani nilipo, inawezekana alinijua jina kwa
sababu naishi nao na wana uwezo wa kujua jina la mtu kulingana na mazingira
yao.
Pia niliwaza kwamba, kuna uwezekano mkubwa yule msichana alitokea
baada ya maono yao kuniona mimi na yule mama wa jirani tukitaka kuwazungumzia
wao kama wapangaji wenye maajabu hivyo hawakupenda iwe hivyo ndiyo maana
msichana akaibuka na kusababisha mvurugano.
“Itakuwa kweli, ndiyo maana yule mama naye alisema ameshajua ni
kwanini aliugua kichwa ghafla, alijua yule msichana ni nani na kwanini yeye
kasikia maumivu ya ghafla vile.”
“Lakini pia kuna wale wauza chipsi, nao niliwakumbuka hasa
yule mmoja aliyesema yule msichana wanamjua, anaishi mtaani, lakini hawajawahi
kubaini anaishi nyumba gani na kwa mzee nani wala anajishughulisha na nini,”
hayo yote niliyawaza mimi.
Nilisimama, nikachukua sabuni ya kuogea ambayo haijafunguliwa,
nikaipiga chini kwenye kapeti kwa hasira huku nikisonya, nikasema kwa
sauti ya chini:
“Humu ndani naishi na majini.”
Kule chumbani nikasikia wakicheka.
“Si unaona, nimesema mimi, lazima naishi nao humu ndani, da!
Najuta sana,” nilisema. Kicheko kikasikika tena, safari hii kilikuwa cha juu
zaidi kuliko kile cha awali.
Moyo ulijaa mawazo, akili ilihisi uchungu wa maisha, niliwaza
fedha nilizozilipa kwa ajili ya kupanga mle ndani, nikamkumbuka dalili,
niligundua alichofanya ni kunitapeli na hakuna lingine wala hakuwa msaada
kwangu.
“Mimi ni mwanaume, kama niliweza kupata fedha za kupanga hapa, sishindwi
kupata nyingine za kupanga sehemu nyingine tena mbali na hapa,” nilisema kwa
moyoni.
***
Usiku nikiwa nimelala, nilichelewa sana kupata usingizi, ghafla
nikaona taswira za watu ukutani, wawili tena wakiwa wamesimama, ni mwanamke na
mwanaume. Niliogopa sana, nikainua kichwa polepole kuwaangalia kwa umakini,
japo kulikuwa na giza, lakini niliweza kuona vizuri lakini si kwa uwazi mkubwa
kama ambavyo taa ingekuwa inawaka.
Ni kweli walikuwa watu wawili kama nilivyoona, tena weupe
nikimaanisha si watu weusi. Walikuwa wakionesha vitendo vya kucheka huku
wakijinyonganyonga.
Kuna wakati walitembea mpaka jirani na kitanda changu kisha
wakageuza na kurudi pale ukutani. Nilipeleka mkono hadi kwenye swichi ya
kitanda (bed switch), nikawasha, cha ajabu sikumwona mtu wala dalili pale
ukutani.
Niliamka nikiwa nahema kwa kasi mpaka nikajishika kifuani,
nikafungua mlango na kutoka nje ili nijifanye nakwenda chooni lengo langu
lilikuwa kupata picha kwa wenzangu kukoje maana niliwashuku wao na wale
walioonekana chumbani kwangu.
Kwa wenzangu niliwasikia wakiroma kwa zamu. Nikajiuliza ina maana
si wao waliokuja chumbani kwangu? Niliona ni utani wa hali ya juu.
Niliamua kurudi chumbani na kukatisha safari ya kwenda chooni,
nikafunga mlango wangu kwa funguo na kupanda kitandani, nilizima taa ili nione
kama yale mauzauza yatatokea tena.
Ukimya ulitawala kwa muda bila kujitokeza chochote, nikaanza
kupitiwa na usingizi kwa kusinziasinzia, ghafla ukutani nikawaona tena walewale
watu wawili.
Safari hii walikuja hadi kitandani, wakakaa, wakasimama, wakaenda
kwenye kabati, wakafungua, wakatoa mashuka na kujifunika, wakayarudisha,
wakaenda nyuma ya mlango, wakatungua mashati yangu mawili, wakagawana na
kuyavaa kisha wakayavua, mmoja mwanaume akaenda sehemu yenye redio, akapeleka
mkono, nikajua anataka kuiwasha, lakini hakufanya hivyo.
Nilichoamua kukifanya akilini ni kuwasha taa kwa ghafla na
kuwavamia na nilipanga kumvamia mwanamke nikiamini ndiye aliyekuja kule kwenye
chipsi. Polepole nilipeleka mkono hadi kwenye swichi, nikawasha taa kwa ghafla
huku macho yangu yakiwa kwao, lakini sikumwona hata mmoja! Kwangu haikuwa
mapambano bali nilichukulia kama changamoto za maisha.
***
Asubuhi, niliamka nikiwa nimechoka sana, lakini kabla sijatoka
kitandani nilisikia nje ya mlango kukiwa na hali ya watu kutembeatembea tena
kwa kasi, niliinua shingo ili nione kama nitasikia zaidi, lakini kukawa kimya.
Niliamka, nikatoka, nilikwenda sebuleni kwanza kuangalia kama kuko
salama. Nilishangaa kukuta mezani kuna mfuko wa rambo uliojaa chipsi kuku kama
nilivyonunua mimi, lakini zangu nilikula, sasa zile sikujua zilitoka wapi.
Niliubeba ule mfuko nikatoka nao, nilifungua mlango mkubwa wan je
nikautupia pembeni kidogo, niliporudi, nikaenda chooni, mlango ulikuwa
umefungwa kwa ndani kwani hata niliposhika kitasa na kukivuta kilikuwa kigumu.
Hii iliashiria kwamba kuna mtu, kwa hiyo moyoni nilisema
nisimame palepale nje ya mlango hadi atoke. Nilisimama eneo ambalo akitoka tu,
uso kwa uso na mimi.
“Tuone leo, wao si wajanja, leo nimemnasa mmoja wao,” nilisema
moyoni.
Dalili zote zilionesha kwamba mle chooni mlikuwa na mtu kwani
niliweza kusikia hata kuhema kwake, mara mlio wa maji, mara alikohoa, tena
kwenye kukohoa nikabaini mtu mwenyewe alikuwa ni mwanamke ndiye aliyekuwa mle.
“We kuhoa mpaka utapike, lakini mimi nipo hapa mpaka utoke,”
nilisema moyoni.
Nilikaa sana, ikafika mahali nikachoka, lakini moyoni nikasema
siondoki hata iweje, lakini nilishtuka kitu, niligundua muda mrefu sijazisikia
zile dalili kama maji au kuhema, nikafunguka akili.
“Mh! Siyo kwamba ametoka?”
Ile namalizia kusema ‘ametoka?’ nikasikia kicheko kutoka kwenye
chumba chao. Vicheko vikubwa sana cha kike na kiume.
Nilirudi chumbani mwili ukinisisimka, hapo ndipo niliamini mia kwa
mia kwamba, nilikuwa nadili na watu wasiokuwa wa kawaida.
Niliingia chumbani, nikampigia simu dalali.
“Haloo,” niliita.
“Haloo. Halooo,” nilirudia lakini sikupokelewa.
Nikiwa nimeachana na simu, mara iliita yenyewe, alikuwa ni dalali
nikapokea.
“Haloo,” niliita.
“Haloo,” niliitikiwa lakini sauti haikuwa ya dalali.
“Mzima bwana?” nilisalimia.
“Tuone leo, wao si wajanja, leo nimemnasa mmoja wao.”
Ha! Nilishtuka sana, nilisikia sauti yangu mwenyewe ikisema hivyo.
Ikaendelea.
“We kuhoa mpaka utapike, lakini mimi nipo hapa mpaka utoke.”
Nilikata simu, nilikuwa nahema sana, mapigo ya moyo yalikuwa
yakienda kwa kasi ya ajabu huku nikishindwa kuona sawasawa.
“Hii ni hatari sasa,” nilisema.
***
Usiku wa siku hiyo sikulala kusema kweli kwani kila nilipofikiria
maisha yale sikuona sababu ya kuendelea kuishi pale. Moyoni nilisema kwamba, ni
afadhali ningeishi na watu ambao ni majambazi kuliko hawa, nafuu ningepanga
nyumba moja na makahaba kuliko kupanga nyumba moja na majini.
Nilichoamua, asubuhi nikifika kibaruani tu niombe ruksa kisha
nianze kumsaka yule dalali na pia nitafute dalali mwingine ambaye atanitafutia
vyumba kwingine na si maeneo yale tena kwani niliyaona yana nuksi.
***
Asubuhi kulikucha salama kabisa, tena usiku wa siku hiyo sikuona
mauzauza wala dalili zake. Nilikwenda kuoga bila kukagua mazingira, moyoni
nilisema liwalo na liwe kwa maana kwamba, wawepo wasiwepo sawa tu.
Bafuni niligundua wameshaoga kwani kulikuwa na majimaji ya muda
mfupi uliopita. Nilipomaliza kuoga, nilijiandaa na kutoka. Nje nilikutana na
mtu ana mkokoteni, akanisalimia.
“Za asubuhi bwana mkubwa?”
“Salama, karibu sana.”
“Asante, kuna watu fulani wanaishi humu nina shida nao.”
Aliposema hivyo nilishtuka sana, niliamini yeye ni mmoja wa wale
ila amejigeuza kwa kujifanya ana shughuli za mkokoteni.
“Unawajua kwa sura?” nilimuuliza huku nikiwa na wasiwasi maana
alinikazia macho.
“Siwajui.”
“Sasa una shida nao kivipi watu usiowajua kwa sura?”
Ni kwamba, kuna binti mmoja huwa wanamtuma niwaletee maji,
nikifika hapa huyo binti anabeba madumu kupeleka ndani, sasa jana nilikutana na
huyo binti nikamuuliza kuhusu malipo yangu ya mwezi sasa, akasema nije
nifuatilie mwenyewe.”
Nilishangaa sana kusikia hivyo. Nijuavyo mimi mle ndani mna watu
wawili, mwanamke na mwanaume, sasa kama kuna binti hilo lilikuwa jipya kwangu,
labda lakini.
“Huyo binti naye anaishi humu au?” nilimuuliza.
“Sidhani, inaonekana kama huwa wanamtuma tu.”
“Kwa nini huamini kama anaishi humuhumu ndani? Hafanani na wao
wenyewe?” hili swali niliuliza likiwa na mtego mkubwa sana, nilitaka nijue
uhalisia wake.
“Siwezi kusema hafanani wakati wao siwajui kwa sura.”
Hapo ndipo nilipopataka, nilidhani atasema hafanani nao, ningejua
ni walewale.
“Oke, nadhani wameondoka kwenda kazini.”
“Ah! Sasa mimi fedha zangu nitazipataje jamani?”
“Subiri wakirudi jioni.”
“Wewe utakuwepo?”
Nililishangaa swali hilo, hakuwa akinidai mimi lakini anataka
niwepo?
“Unataka niwepo?”
“Ee.”
Usikose sehemu ya 04 siku ya jumatano...kuwa nami muda wote Irene Mwamfupe Ndauka
No comments:
Post a Comment