KIKOSI cha Usalama Barabarani jijini Dar es Salaam kimelaumiwa
kwa kuendesha operesheni ya kuzikamata daladala bila ya kufuata
utaratibu na kusababisha usumbufu kwa abiria.
Wakizungumza kwa wakati tofauti jijini Dar es Salaam
juzi, wakazi hao walisema hata kama walikuwa na lengo zuri la kukamata
magari mabovu bado walipaswa kuwa wabunifu, kwa kutafuta utaratibu
mwingine wa kupunguza uhaba wa usafiri.
Mmoja wa wakazi hao, Said Mohamed, alisema operesheni hiyo
iliyoendeshwa mwishoni mwa wiki abiria katika barabara ya Morogoro
ilisababisha abiria kukaa vituoni kwa muda mrefu kutokana na wamiliki
wengi kuondoa magari yao barabarani ili kukwepa kukamatwa.
Hamisi Mohamed, dereva wa daladala, alisema amekuwa akishangazwa na
askari hao, pindi wanapowakamata huwarundikia makosa, ili watoe rushwa
kwa askari hao.
“Utaona askari huyo anakujia kwa vitisho, mara kachukua leseni au
utamuona anang’oa kibao cha namba ya gari, lakini ukishampatia kile
anachotaka analiachia gari,” alisema.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga,
aliwataka wananchi wawe watulivu wakati kikosi hicho kinapotekeleza
sheria ya kuyakama magari mabovu barabarani.
Alitoa wito kwa wananchi kuwa watakapomuona askari aliyekamata gari
bovu halafu katika mazingira yasiyoeleweka akaliachia, wampelekee
taarifa ili askari huyo ashughulikiwe.
Aidha, alimtaka mwadishi kuwasiliana na Ofisa wa Kikosi hicho cha
Usalama Barabarani Mkoa wa Dar es Salaam, Amir Konja, ili ampatie idadi
ya magari mabovu yaliyokamatwa katika zoezi, ambalo limeendeshwa kwa
mafanikio makubwa.
Hata hivyo, Konja alishindwa kutoa ushirikiano tena kama alivyofanya
juzi wakati alipotakiwa kutoa ufafanuzi: “Siwezi kulizungumzia hilo, kwa
bahati mbaya niko hospitali nina mgonjwa”.
No comments:
Post a Comment