KIONGOZI wa msikiti wa Masjid Maftah ulioko Misufini katika
manispaa ya Morogoro, Alhaj Abdul Wazir, maarufu kama Sheikh Koba,
anashikiliwa kwa mahojiano mkoani hapa kwa tuhuma za kumbaka mtoto
mwenye umri wa miaka nane, mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya
msingi Sabasaba.
Taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa
Morogoro, Faustine Shilogile, zilisema mtuhumiwa huyo, anadaiwa kutenda
tukio hilo chumbani kwake, Septemba tatu, majira ya saa mbili usiku,
huko Mbuyuni katika manispaa ya Morogoro.
Mashuhuda wa tukio hilo wakizungumzia mazingira ya tukio hilo, walidai
kuwa Alhaj Koba, amekuwa akiishi nyumba tofauti na mkewe na kwamba siku
ya tukio mke wake alimtuma mtoto wa nduguye kupeleka chakula kwa
mumewe, lakini alichelewa kurudi, hivyo kuamua kumfuatilia kujua
kulikoni.
“Alipofika kwenye nyumba anayoishi mumewe, aligonga na kumuulizia
binti huyo, lakini alielezwa kuwa alishaondoka eneo hilo, lakini mtoto
alijitokeza na kudai alikuwa bado ndani ya nyumba hiyo, na alipohojiwa
kuhusiana na uchelewaji wake, alikiri alikuwa amebakwa hivyo tukio hilo
kuripotiwa polisi,” kilieleza chanzo chetu cha habari.
Polisi walithibitisha kupokea taarifa za tukio hilo, na kwamba
uchunguzi zaidi bado unaendelea ili kumfikisha mtuhumiwa mahakamani.
Katika tukio jingine, kijana Typhory Singa, anashikiliwa na polisi kwa
tuhuma za kumbaka mwanafunzi mwenye umri wa miaka tisa, mwanafunzi wa
darasa la tatu katika shule ya msingi Lipangalala na mkazi wa Liami
Ifakara wilayani Kilombero.
Tukio hilo linadaiwa kutokea Septemba nane mwaka huu, majira ya saa nane mchana.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili mtuhumiwa aweze kuchukuliwa hatua.
CHANZO CHA HABARI NA GAZETI LA TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment