WAREMBO wanaowania taji la Redd’s Miss Tanzania 2013 wametakiwa
kupenda na kuthamini bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya hapa nchini.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Tanzania
Distilleries (TDL), David Mgwassa, wakati akizungumza na warembo
waliotembelea kiwanda hicho kilichopo Chang’ombe jijini Dar es Salaam
mwishoni mwa wiki.
“Nyinyi ni mabalozi wazuri wa kutangaza bidhaa za humu ndani, hivyo
nawaomba sana mzipende na kuthamini sana bidhaa zote zinazozalishwa na
viwanda vya ndani,” alisema Mgwassa.
Alisema kuwa TDL kupitia kinywaji cha Zanzi, imeamua kudhamini
shindano la Miss Tanzania kwa sh milioni 40, lengo likiwa kukitangaza
kinywaji hicho, pia kuboresha shindano hilo.
Mgwassa alisema shindano la Miss Tanzania ni kielelezo muhimu kwa
taifa na kuwataka warembo hao kutangaza vivutio vya utalii nchini kama
Mlima Kilimanjaro, sambamba na kukitangaza kinywaji cha Zanzi kuwa ni
bidhaa bora kwa Watanzania kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi.
Shindano la Redd’s Miss Tanzania linatarajiwa kufanyika Septemba 21,
mwaka huu kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment