Hofu
ya kuchomwa moto kwa Shule ya Sekondari ya Ilboru iliyopo mkoani hapa
imewakumba wanafunzi na walimu hatua ambayo imelazimu kufungwa kwa muda
usiojulikana kuanzia jana, huku uchunguzi wa madai hayo ukiendelea.
Tangazo la kufunga shule hiyo lilitolewa ghafla jana asubuhi na Mkuu wa Shule hiyo, Julius Shila, baada ya kushauriana na bodi, huku polisi wa kawaida wakifanya doria kudhibiti vurugu zozote ambazo zingeweza kutokea.
Wanafunzi wanne wanahojiwa na polisi wilayani Arumeru ili waisaidie kubaini madai hayo, huku wengine 10 wakiwa wamepewa barua za kusimamishwa masomo kwa muda wa siku 21.
Wanafunzi wote watatakiwa kurejea shuleni baada ya kudahiliwa na wakuu wa wilaya zao.
Wanafunzi waliohojiwa na NIPASHE wakiwa wanarudi makwao, waliwahusisha baadhi ya walimu na sakata la kutaka kuchoma shule hiyo.
Walidai kuwa vitisho vya kuchomwa moto kwa shule hiyo vilianza mwaka jana, ingawa polisi walifanya uchunguzi hakuna taarifa zaidi zilizotolewa.
Walisema wiki iliyopita kulikuwa na harufu ya mafuta ya petroli yaliyomwagwa eneo jirani na bweni la shule, tukio ambalo polisi walithibitisha kuwa ni la kweli.
“Baadhi ya walimu walikiri kuhusika, mwaka jana walikubali kuwa shule ilitaka kuchomwa moto, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa hadi sasa na tukio kama hilo limejitokeza tena wiki iliyopita, sasa tunahofia usalama wetu,” alidai mwanafunzi mmoja wa kidato cha tatu.
Hakuna mwalimu yeyote aliyekuwa tayari kuzungumzoa madai hayo ya wanafunzi hao kuwahusisha na njama za kufanya uhalifu huo.
Kaimu Ofisa Elimu wa Mkoa wa Arusha, Sifael Mollel, alisema uchunguzi wa madai hayo unaendelea katika kipindi hiki ambacho shule imefungwa.
Alisema kuwapo kwa hofu hiyo na wasiwasi wa kuzuka vurugu ndiko kulikosababisha shule ifungwe kwa muda licha ya kwamba wanafunzi walikuwa wanaendelea na mitihani.
“Uongozi uliamua wanafunzi warudishwe nyumbani kutokana na hofu ya kuchomwa moto shule, wanafunzi walikuwa wakifanya mitihani kabla ya kuanza likizo fupi, lakini uwapo tishio hilo na kuzuka kwa vurugu, ilionekana ni vema shule ikafungwa,” alisema.
Alisema kwa kawaida likizo fupi ni ya siku 10, lakini kwa tukio hilo wanafunzi hao wamepewa maelekezo ya kwenda kuonana na wakuu wa wilaya zao kwa udahili kabla ya kurejea tena shuleni.
Akizungumzia vitisho vya moto, alisema wanafunzi hao waliwasilisha barua ofisini kwake wakitoa madai kuwa baadhi ya walimu walikuwa wanataka kuchoma moto shule hiyo.
Alisema polisi walienda kufanya uchunguzi Ijumaa iliyopita na kwamba walinusa harufu ya petroli iliyokuwa imemwagwa jirani na bweni.
Kaimu Ofisa Elimu huyo hakutawataja wanafunzi ambao wanahojiwa na polisi wala wanafunzi 10 ambao wamesimamishwa kwa siku 21.
Mkuu wa Shule hiyo, Julius Shila, alikataa kuzungumza na wanahabari kuhusu matukio hayo na hata alipopigiwa simu, alikuwa akiikata mara baada ya mwandishi kujitambulisha.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha polisi kuwapo shuleni hapo wakati tangazo la kufungwa shule hiyo likitolewa, lakini alisema hatua ya kuimarisha ulinzi ililenga kuimarisha usalama.
Shule hiyo ni miongoni mwa shule za serikali za vipaji maalum nchini, ambazo hazina historia ya matukio ya vurugu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment