Habari Hastin Liumba, Nzega.
WANAWAKE wawili wilayani Nzega, mkoani Tabora, wameuawa kwa kukatwa
katwa mapanga katika matukio mawili tofauti yaliyotokana na migogoro ya ardhi na kifamilia.
Tukio la kwanza limetokea katika Kijiji cha Iboja, Kata ya Sigili ambapo
mwanamke mmoja ameuawa kwa kukatwa mapanga kutokana na ugomvi wa
mashamba.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Diwani wa kata hiyo, Pelle Izengo,
alimtaja mwanamke huyo kuwa ni G’wallu Kibunga (55), mkazi wa kijiji
hicho.
Alisema tukio hilo limetokea Septemba 7, mwaka huu, majira ya saa
tatu usiku, ambapo wauaji hao ambao hadi sasa hawajajulikana waliingia
ndani ya nyumba ya mwanamke huyo na kuanza kumshambulia kwa mapanga na
kusababisha kifo chake.
Pelle alisema sababu ya mauaji hayo ni ugomvi wa mashamba ambapo
mwanamke huyo alishinda kesi yake katika Mahakama ya Ardhi Tabora.
Diwani huyo aliwataka wananchi wa kata hiyo kutojichukulia sheria
mikononi, badala yake wafuate sheria ili kunusuru mauaji ya aina hiyo.
Katika tukio la pili, mwanamke aliyefahamika kwa jina la Kundi
Msweya (70), mkazi wa Kijiji cha Mbagwa, ameuawa kwa kukatwa mapanga na
watu wasiofahamika kijijini hapo.
Tukio hilo limetokea Septemba 4, mwaka huu, majira ya saa tano usiku
ambapo watu hao walimvamia ndani na kuanza kumshambulia kwa mapanga
hadi kusababisha kifo chake.
Matukio hayo yamethibitishwa na Jeshi la Polisi huku upelelezi
ukiendelea ili kubaini
waliohusika na mauaji hayo.
No comments:
Post a Comment