WACHEZAJI wa Simba wakiwa kwenye mgomo baridi kushinikiza
kuondolewa kwa Kocha Msaidizi Jamhuri Kihwelo ‘Julio,’ kiungo Henry
Joseph ametemwa kwenye kikosi cha timu hiyo kilichoingia kambini Bamba
Beach, juzi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kujiandaa na mechi za
Ligi Kuu.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo, zinasema kuwa, chanzo cha kuachwa
kwa Henry ni baada ya kusigana na Julio tangu Jumatatu wiki hii wakati
wa mazoezi kwenye Uwanja wa Kinesi, ambapo nyota huyo aligomea mazoezi.
Kuna habari kuwa, Henry alipoulizwa ni kwanini alikuwa kwenye hali ya
kusuasua, akajibu kuwa tayari alishajifua kivyake, jibu ambalo lilimkera
Julio na kumtaka aondoke uwanjani hapo, hivyo kutojumuishwa kambini.
Tanzania Daima ilipojaribu kutafuta kiini cha msigano ndani ya timu
hiyo, baadhi ya wachezaji walikiri Henry kusigana na Julio na kuongeza
kuwa, kuna mgomo baridi unaotokana na wao kukerwa na kocha huyo
msaidizi.
Chanzo hicho kilidokeza kuwa, Julio amekuwa akichukiwa na wachezaji
kutokana na lugha zake za karaha na matusi, ambazo zimekuwa zikiwanyima
raha wachezaji dimbani hasa kwenye mazoezi.
“Hali sio nzuri katika timu yetu, mpaka sasa Henry hayupo kambini
baada ya kutokea mabishano baina yake na Julio, tukiwa mazoezini
Jumatatu,” alisema mmoja wa wachezaji wa timu hiyo ambaye hakupenda
kutajwa jina.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga, alisema
hajui lolote kuhusu suala hilo na kama kuna ukweli, bado ni suala la
kiutendaji zaidi linalohitaji kufanyiwa uchunguzi zaidi kabla ya
kutolewa majibu kwa maslahi ya Simba.
Juhudi za kumpata Julio kutoa ufafanuzi wa kilichotokea kati yake na
Henry, ziligonga mwamba kwani licha ya kutafutwa mara kadhaa kwa siku ya
jana, simu yake haikuwa hewani.CHANZO NI TANZANIA DAIMA.
No comments:
Post a Comment