CHANZO NI GPL
KUFURU! Staa wa filamu za Kibongo, anayepatia zaidi kuigiza kama Mchungaji, Emmanuel Myamba ‘Pastor Myamba’ amefunga ndoa ya kihistoria ambayo imeteketeza mamilioni kuikamilisha, Risasi Mchanganyiko lina sinema nzima.
Emmanuel Myamba ‘Pastor Myamba’na mkewe Praxceda Kassela wakiwa wenye nyuso za furaha baada ya kufunga ndoa.
Pastor Myamba amefunga ndoa na mchumba wake wa muda mrefu aitwaye
Praxceda Kassela mjini Zanzibar, Jumamosi iliyopita, Agosti 2, mwaka huu
na kuhudhuriwa na watu 400.HABARI MEZANI
Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, mmoja wa ndugu wa karibu na Pastor Myamba, alisema ndoa ya ndugu yao ilikuwa ya kifahari na kwamba imevunja rekodi za ndoa za wasanii wote wa Bongo.
“Ilikuwa siyo mchezo, ni ndoa ilivyovunja rekodi na imetumia pesa nyingi sana. Tunashukuru kuikamilisha hili. Mungu ni mwema hakika,” alisema na kuongeza:
“Zimefungwa ndoa nyingi sana za mastaa na kwa kweli kwa umoja wao wameonyesha kufuru kubwa ya fedha lakini kwa hii ya Myamba ni funiko. Hakuna ndoa ya staa yeyote inayoweza kuipiku.”
SASA ANGALIA TOFAUTI
Kufuru ya ndoa ya Myamba inatokana na ukubwa wa gharama za maandalizi, zawadi na hadhi ya harusi yenyewe.
Kati ya ndoa zote za mastaa Bongo zilizofungwa huko nyuma, hakuna hata moja iliyofungwa ufukweni kama alivyofanya Myamba.
NDOA UFUKWENI
Shughuli nzima ilichukua nafasi katika Ufukwe wa Bahari ya Hindi, kwenye Hoteli ya Zanzibar Beach Resort ambapo Mchungaji John Kyashama wa Kanisa la The River of Healing Ministry of Tanzania na wasaidizi wake walilazimika kufika ufukweni hapo na kuwaunganisha wawili hao.
Chanzo kinaendelea kutiririka: “Ilikuwa na utulivu wa hali ya juu. Upepo mwanana ufukweni, huku nyimbo zikiimbwa kwa staili ya kusuuza mioyo. Ni ndoa ya kipekee sana.
“Myamba hakuamini pale Mchungaji aliposema: Sasa nawatangaza rasmi Emmanuel na Praxceda kuwa mume na mke. Makofi na vigelegele vikapigwa. Myamba akamfunua bibi harusi shela.”
SHEREHE BUSTANINI
Baada ya ndoa hiyo kufungwa, shamrashamra zilihamia rasmi katika bustani ya ukweli katika hoteli hiyo ambapo huko kuliandaliwa karamu ya kufa mtu!
Eneo lote la bustani lilionekana kupendeza kwa rangi nyeusi, nyekundu na dhahabu ambazo ndizo zilikuwa rangi kuu za sherehe hiyo.
MSOSI 50,000
Ukiachana na mambo mengine, chanzo chetu kinaeleza kuwa bajeti ya sahani moja ya chakula katika shughuli hiyo ilikuwa ni shilingi 50,000, mbali na vinywaji.
“Ni sahani iliyokuwa na kila kitu. Kwanza chakula chepesi cha utangulizi (starter), halafu kila mtu alipita na kujipakulia mwenyewe (self service) na bado vyakula na vinywaji kibao vilisazwa,” alisema.
MASTAA WANG’ARA
Mastaa mbalimbali wa Bongo Muvi wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania ‘TAFF’, Simon Mwakifwamba walikuwepo kushoo lavu la mwenzao huyo, hivyo kuongeza ladha ya shughuli hiyo.
Mbali na Mwakifwamba, wengine ni Jacob Stephen ‘JB’ (Bonge la Bwana), Salum Mchoma ‘Chiki’ aliyekuwa MC wa shughuli hiyo, Adam Melele ‘Swebe’, Zawadi na wengine wengi.
ZAWADI
Katika kipengele cha zawadi, hapo ndipo kufuru ilipozidishwa, mastaa wa Bongo Muvi peke yao walimzawadia Myamba mifuko ya cement 100, mbali na mastaa wengine waliotoa fedha kivyao nje ya kundi hilo.
Kamati ilifunga kazi kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 250 cash, palepale bustanini ambazo zilipangwa kwenye toroli na kupelekwa mbele kwa maharusi (angalia ukurasa wa mbele).
Mbali na fedha hizo, dada wa Myamba aitwaye Grace Myamba alitoa zawadi ya gari aina ya Nissan Exray lenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100 na kumkabidhi bwana harusi funguo.
PASTOR MYAMBA HUYU HAPA
Juzi Jumatatu, Risasi Mchanganyiko lilimpandia hewani Pastor Myamba na kuzungumza naye kuhusiana na ndoa yake, ambapo alisema anamshukuru Mungu kwa kumfikisha katika hatua hiyo muhimu katika maisha ya binadamu.
“Namshukuru sana Mungu kwani kufunga kwangu ndoa imekuwa ni baraka kubwa katika maisha yangu. Nawashukuru wote ambao wamefanikisha tendo hili muhimu,” alisema Myamba.
FUNGATE HOTELI MBILI
“Najua kuna watu wanaweza kushangaa kwa nini nimeamua kufunga ndoa Zanzibar, ukweli ni kwamba ni kwa sababu wazazi wangu wanaishi huku, sikutaka kuwasumbua ndiyo maana nikawaomba marafiki zangu waungane Zanzibar, nashukuru walinielewa na walifika.
“Hivi ninavyozungumza na wewe tupo honeymoon hapa Zanzibar Beach Resort. Tupo hapa tangu Jumamosi, tutakaa siku mbili zaidi (Jumatano) halafu tutahamia hoteli nyingine ambayo bado hatujapanga. Huenda ikawa nje ya hapa Zanzibar,” alisema.
HONGERENI SANA
Timu nzima ya Risasi Mchanganyiko inawapongeza Myamba na Praxceda kwa hatua hiyo muhimu katika maisha yao na tunawatakieni kila la kheri, Mungu awatangulieni.
No comments:
Post a Comment