HATIMAYE safari ya timu ya Taifa
ya Tanzania, Taifa Stars kuwania tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya
Africa, AFCON 2015 nchini Morocco amefia mikononi mwa timu ya taifa ya
Msumbiji ‘Black Mambas’.
Taifa Stars ikiwa ugenini katika
dimba la Taifa la Zimpeto nje kidogo ya jiji la Maputo imetandikwa mabao
2-1 katika mchezo wa marudiano wa kuwania kupangwa hatua ya makundi ya
kusaka tiketi ya AFCON mwakani.
Katika Mechi ya kwanza iliyopigwa
wiki mbili zilizopita jijini Dar es salaam, vijana wa Mholanzi, Mart
Nooij walitoka sare ya mabao 2-2 na leo hii walihitaji kupata ushindi wa
aina yoyote ile au sare ya kuanzia mabao 3-3.
Matokeo ya jumla baada ya mechi
mbili, Msumbiji wamefanikiwa kufunga mabao 4 na Taifa stars matatu,
hivyo vijana wa Nooij kutupwa nje ya michuano kwa wastani wa mabao 4-3.
Msumbiji walikuwa wa kwanza
kuandika bao la kuongoza dakika za mwisho za kipindi cha kwanza kupitia
kwa Josimar Tiago Machaisse, lakini Mbwana Ally Samatta akaisawazishia
Stars katika dakika ya 77.
Dakika ya 83, kiungo mshambuliaji
wa Msumbiji, mzoefu, mwenye ujanja mwingi wa kupiga chenga na kumiliki
mpira, Elias Gasper Pelembe aliifungia ‘Domingues’ Msumbiji bao la pili
na la ushindi.
Kihistoria Msumbuji wamemekuwa wababe wa Taifa Stars inapofika michezo ya mtoano, hasa kufuzu mataifa ya Afrika.
Mwaka 2007 Stars chini ya kocha
Mbrazil, Marcio Maximo ilifungwa bao 1-0 katika mchezo wa mwisho jijini
Dar es salaam kuwania kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwaka 2008
nchini Ghana na ingeshinda ingefuzu.
Bao pekee la Msumbiji lilifungwa
dakika ya za mapema kipindi cha kwanza na aliyekuwa nahodha wake, Tiko
Tiko akiunganisha kwa kichwa krosi nzuri iliyochongwa kutoka winga ya
kulia na Elias Pelembe.
Mwaka 2012 Taifa stars ilitolewa
tena na Msumbiji kwa changamoto ya mikwaju ya penati katika mchezo wa
kuwania kucheza fainali za kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwaka
2013 nchini Afrika kusini.
Hatua hii ilifikia baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 jijini Dar es salaam na kupata matokeo kama hayo mjini Maputo.
Kwahiyo Msumbiji bado wameendelea kuwa wababe wa Tanzania katika michezo ya mtoano.
Poleni sana Taifa Stars, Poleni Watanzania wote. Mipango mipya inatakiwa kuwekwa.
No comments:
Post a Comment