Akitoa Taarifa ya Mkuu wa Majeshi ya Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Makao Mkuu ya Brigedi Migombani kwa waandishi wa Habari, Mkuu wa Brigedi hiyo Brigedia Jenerali Sharif Sheikh Othman amesema lengo la michezo hiyo ni kujenga mashirikiano kati ya Majeshi na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amesema katika Michezo hiyo kutakuwa hakuna mshindi wala aliyeshindwa na wote watakuwa washindi, lengo ni kujenga uweledi na nidhamu ndani ya majeshi yetu.
“Hii ni fursa ya wanajeshi wetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kukutana pamoja kama tunavyofanya katika mazoezi ya pamoja ya kijeshi”, alisema Brigedia Jenerali Sharif Sheikh Othman.
Amezitaja Nchi za Jumuiya hiyo zitakazoshiriki Michezo hiyo kuwa ni wenyeji Tanzania, Burundi, Rwanda, Kenya na Uganda. Amesema Michezo itakayochezwa na wanajeshi hao ni Mpira wa Miguu, Mpira wa Pete, Mpira wa Mikono, Mpira wa Kikapu na Mbio za nyika na ameelezea viwanja vitakavyofanyika kwa ajili ya michezo hiyo Polisi ziwani ,Vyuo vya Mfunzo Kilimani, JKU Saateni, Pamoja na Viwanja vya Zimamoto na Uokozi.
Brigedia Jenerali Sharif Sheikh ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti wa Michezo hiyo, amewataka Wananchi kujitokeza kwa wingi katika kuona vipaji vitakavyoonyeshwa na wanajeshi kutoka Nchi hizo .
Akitoa ufafanuzi wa Michezo hiyo Leftinenti Kanali Joseph Bakari amesema pamoja na micheo hiyo kutakuwa na Burudani ya Ngoma za Utamaduni kutoka Vikosi vya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Amesema jumla ya wanamichezo 505 wakiwemo Viongozi kutoka Nchi hizo watashiriki michezo hiyo itakayodumu kwa muda ya wiki mbili.
Na Miza Othman Makame Maelezo- Zanzibar .
No comments:
Post a Comment