Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo amewasilisha mswada wa bajeti ya mwaka 1394 (Machi 21 2015-Machi 21 2016) Hijria Shamsia katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani bunge la Iran.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha mswada huo katika bunge, Rais Rouhani amesema, "huu ndio mswada wa pili wa bajeti ambayo imewasilishwa bungeni na serikali yake ya 'tadbiri na matumaini.' Rais Rouhani ameongeza kuwa, kwa mujibu wa mikakati iliyopo mfumuko wa bei nchini utapungua na kufika chini ya asilimi 20.
Rais amesema kati ya nukta muhimu katika kutayarishwa bajeti ya mwaka huu ni utekelezwaji wa sera za 'uchumi wa kimapambano', kupunguza malumbano katika sera za kigeni, kusimamia ipasavyo madeni ya sekta ya umma, kuendelea kutolewa ruzuku kwa wanaostahiki, kupunguzwa mfumuko wa bei sambamba na kuwawezesa wananchi kupata uwezo mkubwa zaidi wa kununua bidhaa na kuboresha huduma za kijamii. Kwa mujibu wa sheria za bunge, wabunge katika Majlisi wana muda wa siku 10 kutoa mapendekezo yao kwa kamati maalumu za bunge. Aidha Rais Rouhani amesema bajeti aliyowasilisha itapunguza utegemezi kwa pato la mafuta ya petroli.
No comments:
Post a Comment