Wikiendi iliyopita, dunia nzima ilikuwa ikiadhimisha siku ya Valentine’s Day au kwa Kiswahili Siku ya Wapendanao! Mambo yalinoga ndani ya Ukumbi wa Dar Live ambapo wakali wa mapenzi, Christian Bella ‘Obama’ na Mzee Yusuf walifanya yao na kuzikonga vilivyo nyoyo za maelfu ya mashabiki waliofurika, Ijumaa Wikienda lilikuwepo kuanzia mwanzo mpaka mwisho.
Mkali wa mapenzi, Christian Bella ‘Obama’ akikonga nyoyo za mashabiki katika usiku wa siku ya Valentine’s Day.
BURUDANI YAANZAPazia la burudani lilifunguliwa na Bendi ya Malaika Music ambapo waliimba na kucheza muziki kwa staili ya kikongomani, wakazikonga vilivyo nyoyo za mashabiki waliohudhuria kabla ya kiongozi wao, Christian Bella kupanda jukwaani na wimbo wake wa Usilie, shangwe zikaibuka kutoka kila kona ya ukumbi huo.
Ukumbi wa Dar Live ulifurika mashabiki wengi katika siku hiyo ya wapendanao.
NANI KAMA BELLA?Bella akiwa jukwaani, alianza kwa kutambulisha bendi yake mpya ya Malaika kisha burudani ikaendelea ambapo alitambulisha wimbo wake mpya uitwao Nashindwa ambao ulipokelewa kwa shangwe za nguvu na maelfu ya mashabiki waliodhuria shoo hiyo ya kipekee.
Burudani ziliendelea ambapo Bella alikamua wimbo wake mwingine wa Msaliti, ukumbi mzima ukafurika kwa shangwe za nguvu, akaendelea kukamua nyimbo zake nyingine na mwisho, akawaomba mabaunsa waliokuwa wakilinda usalama katika ukumbi huo wa kisasa, kuwaruhusu akina mama kupanda jukwaani kwa ajili ya kuimba naye wimbo wa Nani Kama Mama.
Mkali mwingine wa mapenzi Mzee Yusuph akifanya yake stejini.
Ni hapo ndipo umashuhuri wa Bella ulipoonekana kwani akina mama na
wasichana kinbao walipanda jukwaani na kuanza kuimba pamoja Wimbo wa
Nani kama Mama, shangwe za nguvu zikatawala jukwaani hapo na kuweka
historia ambao haijawahi kutokea huku wengi wakilizwa na wimbo huo
kutokana na ujumbe uliomo ndani yake.Wakati watu wengine wakiimba ‘nani kama mama’, nyomi nyingine ilikuwa ikibadilisha maneno na kuimba ‘nani kama Bella’ kuthibitisha kwamba hakuna msanii anayeweza kumfikia katika suala zima la burudani.
Baada ya kukamua sana, Bella pia alikumbushia enzi za zamani alipokuwa na Akudo Impact kwa kuimba wimbo wa Bomoabomoa ambao nao uliziguza hisia za wengi, akashuka jukwaani huku mashabiki wakionekana kuwa na hamu kubwa ya kuendelea kusikiliza nyimbo zake.
Mwandishi wetu alimfuata Bella na kuzungumza naye mawili matatu:
Mwandishi: Shoo yako imekubalika sana, watu wamecheza na kufurahi mno, unalizungumziaje hili?
Bella: Muziki ndiyo kazi yangu, nimekuja kufanya kazi kwa hiyo nikiona mashabiki wanakubali kazi zangu, nafurahi sana.
Mwandishi: Unafikiri kuna msanii gani wa kushinada na wewe?
Bella: Mimi sijaja kushindana na mtu yeyote ila nimekuja kuwapa mashabiki wangu ile kitu wanataka. Nataka waupende muziki wangu.
MZEE YUSUF ACHA KABISA
Baada ya Bella kushuka jukwaani, iliwadia zamu ya mfalme wa muziki wa mwambao Bongo, Mzee Yusuf ambaye naye alifanya shoo ya nguvu na kuweka historia ya aina yake akiwa na Bendi ya Jahazi Modern Taarab. Nyimbo zao kibao za mapenzi zilishangiliwa kwa nguvu mpaka usiku mnene.
MSASANI CLUB NAKO KULIPENDEZA
Wakati huohuo, burudani nyingine ya nguvu ilikuwa ikiendelea katika Ukumbi wa Msasani Club jijini Dar es Salaam ambapo wasanii lukuki walikuwa wakikamua shoo ya nguvu wakiwemo Msaga Sumu ambaye alikamua nyimbo zake kibao ukiwemo Shabiki wa Yanga ulioshangiliwa kwa nguvu, hasa ukizingatia kuwa timu hiyo ilikuwa imepata ushindi kwa kuifunga BDF XI FC ya Botswana kwa mabao 2-0.
Burudani iliendelea kwenye ukumbi huo ambapo baada ya Msaga Sumu kushuka, timu ya Radio EFM ikiongozwa na DJ Majay na Sebo ilipanda jukwaani kabla ya kumpisha mamaa wa majanga, Snura kufanya yake. Baada ya Snura alipanda Recho ambaye alizua gumzo kwa kuvaa kinguo kifupi kilichoacha wasi sehemu kubwa ya maungo yake.
Alipotaka mtu mmoja apande kucheza naye jukwaani, njembammoja ambaye hakufahamika jina lake, alipanda na kuanza kumbeba juujuu msanii huyo na kusababisha mashabiki waanze kumwagia pombe njemba huyo nakumtaka amuache Recho aendelee kutumbuiza.
Burudani ziliendelea ambapo mpaka Ijumaa Wikienda linaondoka ukumbini hapo, shangwe zilikuwa zinaendelea kutawala.
No comments:
Post a Comment