Yule ambaye hathamini penzi huwa anakuwa na sababu zake. Zinaweza kuwa za msingi au zisiwe na msingi. Anaweza kuwa hathamini kwa sababu ana mchumba wake mwingine kama si mke au mume. Hiyo ni sababu ya msingi lakini awe ameisema mapema kabla safari ya uhusiano haijafika mbali.
Anaweza kuwa hathamini kwa sababu hayuko tayari wakati huo kuishi na mtu. Anachoamini yeye ni kwamba muda wake wa kuwa ‘serious’ na mapenzi bado haujafika. Hiyo si sababu ya msingi sana lakini wapo watu wa aina hiyo.
Kwa makusudi kabisa mtu anaamua kucheza na akili ya mwenzake kwa kujifanya ana penzi la dhati kumbe moyoni ana lake jambo. Mtu wa aina hiyo huwa hawezi kudumu muda mrefu na mwenzake kwani uongo siku zote haujifichi, utadhihirika tu!
Kuna mwingine anaweza kuwa na wewe kwa sababu tu ya maslahi. Anajifanya anakupenda kumbe moyoni anakuwa na lake jambo. Utafika wakati atakapotimiza anachokihitaji basi atamuoa au kuolewa na mtu anayemtaka.
Bahati mbaya sana, katika aina ya watu ambao wanacheza na mioyo ya watu, upande wa wanaotendewa huwa haujui lolote. Watu hao wanacheza na mioyo ya wenzao kwa kipindi fulani halafu baadaye wanakuja kufanya maamuzi mengine.
Upande wa pili mwenzake anaanza kuteseka. Kwa sababu alishawekeza nguvu kubwa penzini, alishajiwekea matarajio yake kwamba penzi lao litafika kwenye hatua ya ndoa na kudumu zaidi kumbe mwenzake hana mpango huo.
Kwa sababu alikuwa na penzi la kweli, hayupo tayari kukupoteza. Ataanza kulazimisha kwa namna yoyote atetee penzi lake. Atapambana kwa kila namna lakini zaidi atakayoyapata ni maumivu. Kila atakalolifanya kwake litakuwa ni mateso.
Kinachotakiwa kufanywa na wewe unayeteseka kwanza, unatakiwa kuyakubali mateso na kuyaona ya kawaida.
Yachukulie kama ni sehemu ya changamoto za maisha na kuanza kutafuta suluhu ya haraka ili moyo wako usiumie zaidi.
Kama umeshafanya kila liwezekanalo ukaona bado hakuelewi, huna sababu ya kuanza kunung’unika. Tuliza akili yako na ikiwezekana tafuta vitu vya tofauti ufanye ambavyo vitakufanya uondoke kwenye mawazo hayo.
Usitumie muda mwingi kuwaza umbali wa safari yenu mliyopitia maana kwa mtu aliyeamua kufanya yake hawezi kutambua maumivu utakayoyapata. Kwa nini uumie moyoni kwa kulilia penzi ambalo mwenzako halithamini hata chembe? Kwa nini uumie kwa mtu ambaye hajawahi na hatarajii kuthamini penzi lako? Kwa nini uumie kwa mtu ambaye tayari ana chaguo lake? Achana naye.
No comments:
Post a Comment