Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Machozi Entertainment, Gadner G Habash, wasanii hao ambao watatumia bendi katika kuonesha umahiri wao, wamejumuika kwenye shindano hilo ili kukidhi kile mashabiki wa Miss Ilala wanachotarajia.
Habash aliwataja wasanii hao wa muziki wa kizazi kipya kuwa ni Jaydee, Ommy Dimpoz, Banana na Chegge.Alisema, mbali ya wasanii hao, msanii wa runinga, Steve Nyerere, ndiye atakayeliongoza shindano hilo kama MC.Mkurugenzi huyo alisema, vimwana 14 wanatarajiwa kupanda jukwaani kuwania umalkia wa Redd’s Miss Ilala 2012 na 12 kati yao, wiki iliyopita walishindana kwenye shindano la kipaji ambapo watano walitinga hatua ya fainali, ambayo itamaliziwa siku ya shindano lenyewe, Ijumaa.
“Katika kinyang’anyiro hicho, mrembo Mary Chizi alikuwa kivutio zaidi kwa jinsi alivyoonesha umahiri wake wa wepesi wa kujivingirisha mwili huku Mectilda Martin akizoa ukumbi mzima, kwa ‘kurap’ na huku akiwa ameendana kwa kucheza, hata mavazi yanayotumiwa na wasanii wa miondoko hiyo,” alisema Habash na kuongeza.
Magdalena Munisi naye hakuwa nyuma katika kumwigiza mwanamuziki nguli wa Marekani, Ciara, kwa umahiri wake wa kulitumia jukwaa, lakini kubwa kuliko, pia kwa mrembo Amina Sangawe, aliyebuni nguo kwa kutumia vipande viwili vya khanga, ambapo aliviunganisha jukwaani kupitia pini na kumvika mrembo mwenzie. Stella Morris kwa upande wake alionesha ukali kwa kuimba.
Habash alisema warembo hao, wamekuwa wakijifua kwa takriban wiki nne chini ya wakufunzi, Slyvia Mashuda ambaye ni Miss Tanzania namba mbili 2008 na Miss Ilala mwaka huo, Neema Mbuya na Dickson Daudi wa THT katika shoo.
Alibainishwa kuwa, Miss Ilala, yenye rekodi ya kutoa warembo wanne waliotwaa taji la Miss Tanzania kuanzia mwaka 1999, (Hoyce Temu), 2000 (Jacqueline Ntuyabaliwe ‘K-Lyne’, 2002 (Angela Damas), na Salha Israel anayeshikilia taji hilo kwa sasa, imepania kuendeleza rekodi yake nzuri mwaka huu.
Redd’s Miss Ilala inadhaminiwa na City Sports Lounge, Redd's Premmium Cold, Uhuru One, Dodoma Wine, Nyumbani Lounge, gazeti la Jambo Leo, 100.5 Times FM, 88.4 Clouds FM na Amaya Salon.
No comments:
Post a Comment