Na George Kayala
MCHUNGAJI wa Kanisa la Glory of God Miracle Center, Peter Rashid Aboubakar (pichani), ametupiwa skendo kisha yeye mwenyewe akakiri kuoa mwanaume mwenzake.
Peter ambaye mwenyewe hupenda aitwe mtume, ameshuhudia mbele ya Uwazi kwamba ni kweli alioa mwanaume lakini ni zama ambazo alikuwa hajaokoka wala kupata upako wa kuongoza kanisa.
Awali, Uwazi lilipokea taarifa kutoka kwa vyanzo vyake kwamba Peter na utumishi wa Mungu wapi na wapi, kwa maana ana rekodi za uchafu, ikiwemo kuishi kinyumba na mwanaume mwenzake.
Chanzo chetu kilidai kuwa Peter alimuoa mwanaume mwenzake anayeitwa Abdallah Athuman na waliishi wote Ilala, Dar es Salaam.
ALICHOKISEMA MTUME PETER
Mchungaji huyo alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo alijibu: “Kwanza hiyo siyo skendo. Huyo Abdallah Athuman Hamis, ni kweli nilimuoa, hata kwenye ushuhuda wangu nimeeleza, kwa hiyo siyo jambo la siri.”
Peter aliendelea kusema, alitoa ushuhuda mzito kwenye mkanda wa video uliopo kwenye DVD, akieleza matukio yake mengi aliyowahi kuyafanya kabla hajaokoka, likiwemo hilo la kuoa mwanaume mwenzake.
“Ndani ya huo mkanda wa video nimeeleza kwamba kabla sijaokoka nilikuwa mchawi, nilikuwa na wake wanne. Watatu ni wanawake na mmoja ni mwanaume, tena kwa sababu nilikuwa nampenda sana, nilimjengea nyumba Ilala,” alisema Peter na kuongeza:
“Niliishi naye kwa miaka sita. Mwaka 1998 niliachana naye baada ya kuokoka. Kwa hiyo siyo tu kuoa mwanaume, mimi nilikuwa mchawi kwelikweli wakati sijaokoka.”
KILICHOPO NDANI YA DVD
Timu ya Uwazi, ilitazama mkanda huo wa video na kubaini mambo kadhaa ambayo Peter aliyatolea ushuhuda:
Aliua na kula nyama za watu kwa njia za kichawi.
Alikuwa bosi wa wachawi ukanda wa Afrika Mashariki. Cheo hicho amedai alipewa chini ya bahari na Lucifer (Shetani).
Aliua mke wake wa kwanza na watoto kwa kuwatoa kafara ili atunukiwe mamlaka kwenye himaya ya wachawi.
Chanzo cha kuokoka kwake ni maradhi ya mkewe kupata hedhi isiyo na kikomo.
Alizaliwa kwenye ukoo wa wachawi, akasomea fani hiyo ya ushirikina na kufuzu kwa alama za daraja la juu.
No comments:
Post a Comment