Mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia amewahonga wabunge kadhaa wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, JAMHURI imethibitishiwa. Habari za uhakika kutoka kwa baadhi ya wabunge na Ofisi ya Spika zinasema kwamba rushwa hiyo ilitolewa kama “asante” kwa wabunge hao baada ya kuzuru moja ya vitegauchumi vya mfanyabiashara huyo kilichopo Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam, wiki kadhaa zilizopita.
Mfanyabiashara huyo, ambaye ni mpenzi wa michezo nchini, pamoja na kuwahonga wabunge, amekuwa akituhumiwa kuwaweka baadhi ya waandishi wa habari kwenye malipo ya kila mwezi. Mkakati huo umemsaidia kutoguswa na vyombo vingi vya habari.
Miongoni mwa wabunge wanaotuhumiwa kupokea hundi ya Sh milioni moja kutoka kwake ni Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala; Pindi Chana. Hata hivyo, mbunge huyo amekataa kukubali au kukanusha taarifa hizo zinazoihusu Kamati yake.
Habari zaidi zinasema baadhi ya wabunge walipokea hundi, lakini baadaye wakashituka na kuzisalimisha katika Ofisi ya Spika. Pamoja na Kamati hiyo, kuna habari kwamba wajumbe wa Kamati nyingine kadhaa nao walialikwa na kupewa kitita cha fedha. Hundi hizo ziliambatanishwa na barua za kuwashukuru wabunge hao kwa kuzuru eneo hilo la biashara.
Lakini cha kushangaza ni kwamba hata wabunge ambao hawakushiriki ziara hiyo, nao wanadaiwa kupelekewa hundi za Sh milioni moja kila moja, na barua za shukrani. Hatua hiyo, pamoja na kutokana na msukumo wa kimaadili miongoni mwa wabunge hao wachache, inaelezwa kwamba ilitokana na hofu ya vita dhidi ya rushwa iliyowaingia wabunge.
“Baadhi ya wabunge waliona hili ni ‘bomu’, wakaamua kusalimisha hundi hizo kwa Spika, lakini wengine wakatulia nazo,” amesema mbunge mmoja. Miongoni mwa waliokataa mwaliko na hundi hizo ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema). “Nakuhakikishia kuwa sikupokea, mimi ni masikini jeuri, nilikataa kwenda kwa sababu nilijua ni masuala ya rushwa,” amesema Mdee.
Mwingine anayesemekana kuzikataa fedha hizo ni Mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes (CCM). Chanzo cha habari kinasema aliwasihi mno wabunge wenzake kuepuka kitendo hivyo haramu. Alipoulizwa na JAMHURI kwa njia ya simu, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alikwepa kuzungumzia suala hilo kwa maelezo yake kwamba alikuwa katika ziara ya kiofisi nchini Srilanka na hivyo akamtupia mzigo huo Katibu wa Bunge.
“Hii tabia ya mtu kuwa mbali anazungumzia mambo ya Dar es Salaam si nzuri, mimi niko Srilanka kwenye mkutano… mtafute Katibu wa Bunge, sipendi majungu hata siku moja,” alisema Spika Makinda kwa ghadhabu. Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, juhudi za kuwasiliana na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, hazikuzaa matunda baada ya JUMHURI kumpigia simu yake ya mkononi mara kadhaa ikiita bila kupokelewa.
Wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ni Chana (Mwenyekiti), John Lwanji (Makamu Mwenyekiti), Abbas Mtemvu, Nimrod Mkono, Halima Mdee, Fakharia Khamis Shomar, Zahra Ali Hamad, Mussa Haji Kombo, Felix Mkosamali, Blandes, Azza Hilal Hamad, Mustapha Akunaay, Jaddy Simai Jaddy, Tundu Lissu, Deogratias Ntukamazina, Jason Rweikiza, Rashid Ali Abdallah, Mohamed Said Mohamed, na Dk. Haji Mponda.
Hivi karibuni, Spika Anne Makinda alilazimika kuivunja Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini baada ya wajumbe wake kadhaa kutuhumiwa kupokea rushwa ili wakwamishe Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ya mwaka 2012/2013. Pamoja na kuivunja, Spika aliagiza uchunguzi wa tuhuma dhidi ya wabunge hao uanze mara moja ili watakaobainika waweze kuwajibishwa. Pia aliahidi kuzifumua Kamati nyingine zenye vimelea vya rushwa.
Ni dhahiri kuwa suala la rushwa bungeni sasa linaelekea kuwa jambo la kawaida. Rushwa imekuwa ikitolewa kwa baadhi ya wabunge, kwa ajili ya kusaidia kupitishwa kwa bajeti na hoja mbalimbali zenye masilahi kwa makundi ya wafanyabiashara.
Uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki uliofanyika Aprili, mwaka huu, uligubikwa na rushwa ya wazi wazi. Licha ya vyombo vya habari kuandika na kutangaza habari hizo, hakuna hatua za dharura zilizochukuliwa kudhibiti hali hiyo.
No comments:
Post a Comment