Wamesema kutokana na adhabu wanayoipata kwa kukaa gerezani, wametubu makosa yao kwa Rais Kikwete na pia wanamuomba awaombee msamaha kwa jamii ya Watanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
Walisema hayo kupitia barua yao ya wazi yenye anuani: Gereza Kuu Maweni Tanga, P.O.Box 5078, Tanga, waliyoiandika kwa Rais Kikwete.
“Mheshimiwa Rais tunakuomba urudishe moyo wako nyuma na utukumbuke hata sisi watoto wako, ambao tulikukosea makosa makubwa. Na pia tunakuomba utuombee msamaha kwa jamii nzima ya Watanzania wote,” walisema wafungwa hao na kuongeza.
“Mheshimiwa Rais tukirejea katika vitabu vya Mwenyezi Mungu vinasema kwamba, mwenye kukosa kosa lolote na baadaye akatubu mbele ya Mwenyezi Mungu humsamehe.”Maelezo ya barua yao hiyo waliyatuma kwa NIPASHE kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms) juzi.
Walisema wao ni wafungwa katika gereza hilo wanaotumikia adhabu ya vifungo virefu, lakini wanajihisi kama wametengwa na hawastahili kupewa msamaha kana kwamba, si Watanzania.Walidai mwaka 1996, Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, alitoa msamaha kwa wafungwa wa vifungo virefu nchini kote, lakini tangu Rais Kikwete aingie madarakani hawajakumbukwa katika msamaha wa Rais.Walidai kila inapofika vipindi vya msamaha katika Sikukuu ya Uhuru, wafungwa wanaopewa msamaha ni wale tu wanaotumikia vifungo vinavyoanzia miaka mitano kurudi chini, lakini wale wanaoanzia vifungo vya miaka sita na kuendelea, hawaguswi na msamaha wa Rais.
“Mheshimiwa Rais, tunakuomba utambue kwamba, sisi wafungwa wote tuliopo magerezani ni raia wa Tanzania na sisi wote tunakutegemea wewe, kwani ndiye mlezi wetu na baba yetu,” walisema.Walisema Machi 16, 2006, Rais Kikwete alitembelea Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam na kujionea namna wafungwa wanavyoishi kwa tabu gerezani, ukiwamo kulundikana katika sehemu za kulala.
No comments:
Post a Comment