Moto huo ulitokea juzi baada ya watu wasiofahamika kuchoma shule hiyo, ambayo inamilikiwa na kanisa Katoliki misheni ya Ulete.
Wakizungumza na MTANZANIA kuhusu tukio hilo wananchi wa kijiji cha Lumuli, walisema hali hiyo inakatisha tamaa kwa wanafunzi kuendelea na masomo, huku wao kama wazazi wamejawa na hofu juu ya maisha ya watoto wao.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho Estelina Ngubi, alisema kuna haja kwa Serikali kusaidia uchunguzi wa matukio ya moto shuleni hapo, kwani yamekuwa yakitokea mara kwa mara.
Alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha hasara kwa wanafunzi na shule, jambo linalovunja moyo wa kuendelea na masomo yao.
Kwa upande wake Michael Msofu, alisema moto huo una sura tata, kwani ni hali inayojenga imani za kishirikina miongoni kwa wakazi wa eneo hilo.
“Huo moto kwa sisi wahehe huwa tunauita Kiwaya, yaani moto unaoteketeza mara moja bila kujua umetokea vipi, hii inatokana na aina ya moto wenyewe.
“Kila tunapogundua kuwa hapa panamoto, unapoanza kuzima, tayari huwa mkubwa na huteketeza kila kitu hivyo hiki ni kiwaya,” alisema Msofu.
Akielezea chanzo cha moto huo shuleni hapo, Mkuu wa shule ya hiyo Matholinus Kibuga, alisema katika kipindi cha miezi miwili umewashwa mara mbili na kuteketeza vyumba vitano vya mabweni ya wanafunzi wa kiume.
Kibuga, alisema kutokana na moto huo hasara iliyopatikana ni zaidi ya Sh milioni 80.4, hali iliyofanya wanafunzi wake kukosa la kufanya baada ya vifaa vyao kuteketea.
“Awali shule yetu ilipoungua chumba kimoja cha bweni la wasichana kiliteketea na kusababisha hasara ya Sh milioni 9. Hata hivyo moto huu wa safari hii umesababisha harasa ya kuteketea kwa majengo, Vitanda, vitabu, nguo na madaftari, pamoja na mali za wanafunzi na vifaa vya shule.
Kutokana na ajali hiyo ya moto, ilimlazimu Waziri wa Fedha Dk. William Mgimwa kutembelea shule hiyo ambapo alijionea madhara yaliyosababishwa na moto huo.
Dk. Mgimwa, ambaye pia ni Mbunge wa Kalenga (CCM), aliwataka wananchi wa eneo hilo, kuhakikisha wanawafichukua watu waliohusika na tukio hilo.
Mbali na agizo hilo, Dk. Mgimwa alikabidhi msaada wa vifaa vya ujenzi vyenye dhamani ya Sh milioni 5, ili kuweza kusaidia ukarabati wa majengo hayo.
Vifaa hivyo vilivyokabidhiwa ni pamoja na bati 150, Saruji mifuko 100 pamoja na rangi makopo 30.
Kutokana na kutokea kwa moto huo shuleni hapo shule hiyo imelazimika kufungwa, ili kupisha ukarabati wa majengo hayo.
Chanzo: Mtanzania
No comments:
Post a Comment