KUNA taarifa za kutatanisha kuhusu afya ya Spika wa Bunge, Anne
Makinda, ambapo inadaiwa kuwa amelazwa katika Hospitali ya Apollo nchini
India.
Habari za ambazo gazeti hili limezipata toka nchini India kwa watu
wake wa karibu, zimeeleza kuwa Spika amelazwa tangu wiki iliyopita
katika hospitali hiyo.
Vyanzo vyetu hivyo vilisema, Spika Makinda ameongozana na watu watano ambao wamekuwa wakionekana naye hospitalini hapo.
Hata hivyo, gazeti hili halikuweza kufahamu mara moja ugonjwa
unaomsumbua kutokana na jambo hilo kuwa siri kati ya mgonjwa na
madaktari wake.
Taarifa za ndani zinasema kuwa baadhi ya watu waliofika kumuona waliambiwa kwamba anasumbuliwa na macho.Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, alikiri kuwa Spika alikwenda nchini humo kwa shughuli mbili ikiwamo ya kufanya uchunguzi wa afya wa kawaida.
Alisema Makinda alikwenda nchini humo mwanzoni mwa mwezi huu kwenye
mkutano wa Maspika Wanawake (IPU) na baada ya kumaliza shughuli hiyo
ndipo akaenda kufanya uangalizi wa afya yake.
Kashilila ambaye hata hivyo alikwepa kuzungumzia kama Spika amelazwa, aliishia kusema tu kwamba alipitia kufanya uangalizi wa kawaida wa afya yake na amekuwa akifanya hivyo kila mwaka.
Kwa mujibu wa Kashilila, Spika atarejea wiki ijayo baada ya kumaliza taratibu zote za kuangalia afya yake.
Wakati Dk. Kashilila akisema hivyo, mitandao mbalimbali ya intaneti,
ilionyesha kuwa mkutano huo wa maspika wanawake ulifanyika kati ya
Oktoba 3 hadi 4 mjini New Delhi, nchini humo.
Hivyo, endapo Spika alitoka kwenye mkutano na kupitia moja kwa moja
kuangalia afya yake, atakuwa ametumia takriban siku 11 hadi kufikia leo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoandikwa kwenye mitandao ya intaneti, katika mkutano huo ambao mada kubwa iliyokuwa ikijadiliwa ni masuala ya jinsia, Spika Anne Makinda, alichangia kuhusu suala hilo akisema wanawake maspika wana jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba mabunge yanazingatia ujinsia.
Akichukulia mfano hatua ambazo Tanzania imechukua katika kufanikisha
masuala ya kijinsia katika Bunge, Makinda alielezea umuhimu wa maspika
wanawake kuhakikisha suala hilo linafanyika kwa vitendo ikiwa ni pamoja
na kuanzisha kamati ya usawa wa kijinsia pamoja na suala zima la bajeti
sanjari na kuimarisha muundo wa mabunge.Habari na Ratifa Baranyikwa.
No comments:
Post a Comment