Akihutubia katika kilele cha kuzima Mwenge wa Uhuru, sherehe zilizokwenda sambamba na kumbukumbu za maadhimisho ya miaka 13 ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, mjini Shinyanga, Rais Kikwete alisema amechukizwa na hatua za watu kujichukulia sheria mkononi.
Kauli ya rais inakuja ikiwa ni siku tatu tangu vurugu kubwa kutokea eneo la Mbagala Kizuiani jijini Dar es Salaam na kusababisha makanisa saba na magari kadhaa kuharibiwa, baada ya mtoto Emmanuel Josephat (14) kudaiwa kukojolea kitabu hicho kitakatifu kinachotumiwa na Waislamu.
Rais Kikwete aliwaeleza wananchi kuwa ametembelea eneo hilo na kusisitiza kuwa kitendo hicho cha viongozi wa dini kuwahamasisha wafuasi wao kujichukulia sheria mkononi hakikuwa sahihi, kwa sababu kijana huyo alifanya tendo hilo bila kushurutishwa na kundi wala mtu yeyote.
Aliongeza kuwa iko haja ya wafuasi hao kujizuia na kutuliza hasira zao kwa kutafakari kwanza kwani hata kijana mwenyewe tayari alikuwa mikononi mwa Jeshi la Polisi.
“Kitendo cha kundi hilo la waumini wa Kiislamu kuingilia kazi za vyombo vya dola hakikuwa sahihi, kwa sababu kimesababisha mambo ya kusikitisha na yasiyokuwa na maelezo ya kujitosheleza ndani ya jamii.
“Niliwasihi kuwa pamoja na hasira walizokuwa nazo wawe na subira na kuvumiliana wakati viongozi wa dini zote mbili wanapojiandaa kukutana na kufikia muafaka,” aliongeza.
Rais Kikwete aliwataka wananchi wajiepushe na vitendo vya kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani katika nchi, hivyo akawashauri wasichukue uamuzi wa hasira wakati wa tatizo kwa sababu kwa vyovyote vile ni lazima watadondokea kwenye makosa.
Alisema vijana 122 wanaodaiwa kutoka kundi la harakati za Kiislamu wakiwemo 36 vinara wakuu wa vurugu hizo, wanashikiliwa na polisi.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete aliwahamasisha Watanzania kuendelea kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwenye tume inayoratibu maoni bila kushawishiwa kwa ulaghai wa aina yoyote, kwamba hiyo ni haki na utashi wa kila mtu.
Akemea rushwa
Rais Kikwete katika hilo, aliwataka wananchi wote kuchukua jukumu la kupambana na vitendo vya rushwa pasipo kuwaachia kazi hiyo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Alisema vita hiyo ni ya kila mtu huku akiwapiga vijembe wale wanaolalamika uwepo wa vitendo hivyo pasipo kuchukuwa jukumu la kuwataja hadharani wahusika ili wachukuliwe hatua.
“Kama tunaendelea kulalamikia rushwa bila kuwataja wala rushwa haiwezi kutusaidia kuitokomeza. Rushwa ni hatari hasa inapoingia hata kwenye vyombo vya kusimamia sheria na kutoa haki,” alisema.
CCM watoa kauli
Wakati huo huo, Chama Cha Mapinduzi, kupitia kwa Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kimelaani vurugu za kidini zilizotokea Mbagala Kizuiani.
Alisema kuwa CCM kinalaani tukio la kukojelewa kwa kitabu kitakatifu cha Kuran na vile vile vitendo vya kuvamiwa na kuchomwa moto makanisa na uporaji wa mali, akisisitiza kuwa havifanani na mila na desturi za Watanzania.
“Kitendo cha kukojolea kitabu kitakatifu cha Waislamu hakikubaliki, na kitendo cha kuvamia na kuchoma moto nyumba za ibada za Wakristo na kufanya vurugu pia hakikubaliki,” alisema Nape.Via Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment